Na Okuly Julius _ Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera, amezitaka taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kufanya kazi Kisekta ili kuweza kuwa na matokeo makubwa katika Mageuzi ya elimu nchini.
Ametoa Maelekezo hayo Novemba 25, 2024 jijini Dodoma, wakati akifunga Mafunzo Elekezi ya siku tatu kwa Maofisa Uthibiti ubora wa Wilaya Wateule ikiongozwa "Kaulimbiu inayosema Uthibiti Ubora wa Shule unaozingatia Weledi, Maadili na Uwajibikaji kwa matokeo chanya ya ujifunzaji"
" ukitaka kufanikiwa katika Sekta hii ya elimu ni lazima uhakikishe unafanya kazi Kisekta yaani kwa kushirikiana na Idara za elimu na sekta nyingine ambayo inatoa elimu na hayo ndio maelekezo ya Serikali ili kupata matokeo Makubwa katika Ubora wa Elimu na sio lazima kufanya kazi kama Wizara," ameeleza Mahera
Dkt. Mahera amewataka Wathibiti Ubora hao kuhakikisha wanatumia fedha kidogo walizonazo kuleta matokeo kwani Serikali inategemea matokeo zaidi kutoka kwao.
" ukifanya kazi nzuri hata hao unaowafanyia watakufurahia na maendeleo yako yataonekana kwani kila mmoja atakuwa an Ashuhudia, hata zikitokea nafasi za Juu unaweza ukajumuishwa na hayo ndio matunda ya kuwatumikia vyema wananchi na nafasi uliyekasimiwa kikamilifu,
"Nimefahamishwa kwamba mmejifunza mambo mengi katika mafunzo haya ambayo ni pamoja na; Wajibu wenu katika usimamizi wa utekelezaji wa Mitaala iliyoboreshwa; Maeneo muhimu ya Kiunzi cha Uthibiti Ubora wa Shule yaliyoboreshwa kulingana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya Elimu; Mfumo wa uthibiti ubora wa Shule, muundo wake na namna utakavyotumika pale utakapokuwa tayari; taratibu za manunuzi ya Umma kwa kutumia mfumo wa NeST,
"Aidha, nimefahamishwa pia mmejadili kuhusu matumizi ya mfumo wa usajili wa shule (SAS), masuala ya taratibu za fedha, masuala ya Sheria ya Elimu na yahusuyo utawala na uendeshaji wa ofisi zenu. Ni matumaini yangu kuwa mlitumia muda wenu vizuri na nategemea maarifa na stadi mlizojifunza zitawapatia weledi katika kuzifanya kazi zenu na kuwa chachu ya kuongeza uwajibikaji,"ameeleza Mahera
Dkt. Mahera amesema Uthibiti Ubora wa Shule ni chombo muhimu cha kutathmini ufanisi wa shule na vyuo vya ualimu katika mchakato mzima wa ufundishaji na ujifunzaji.
Hivyo, Wajibu huo unawataka wathibiti ubora kuzisaidia Taasisi wnazozifanyia tathmini ili ziweze kufikia viwango vya Ubora vilivyowekwa na nchi. Hivyo, ni muhimu sana kujiongezea ujuzi na maarifa kila wakati pengine pasipo kusubiri mafunzo kama hayo kutokana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
"Ni vema kuwa na jitihada binafsi za kujiongezea maarifa kupitia fursa nyingine za kutumia kwa manufaa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia duniani na ya mitandao mbalimbali," amesisitiza Dkt. Mahera
Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule Ephraim Simbeye amesema Wizara ya Elimu kupitia Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule, imefanikiwa kutekelezaji maboresho ya Muundo wa Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule ambapo kwa sasa muundo unawatambua Maafisa Uthibiti Ubora wa Wilaya, cheo chenye majukumu ya waliokuwa Wathibiti Wakuu Ubora wa Shule (W1)
"Kufuatia maboresho ya Mitaala ya Elimumsingi, Wizara imeboresha Kiunzi cha Uthibiti Ubora wa Shule cha Mwaka 2017 na Miongozo yake ili viendane na matakwa ya mitaala ," amesema Simbeye
Pia Simbeye amewataka wathibiti ubora nchini kulinda miundombinu na rasilimali walizokabidhiwa ili ziweze kuwasaidia katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza katika utendaji kazi wao.
No comments:
Post a Comment