Mkuu wa mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga akiongea na Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali baada ya kupokea ugeni kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ofisini kwake, Babati mkoa humo, leo, tarehe 16 Desemba, 2024.
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, kutoka REA, Mhandisi, Advera Mwijage akitoa taarifa kuhusu Mradi wa usambazaji mitungi ya gesi ya kilo 6, ambayo itaanza kusambazwa kwa Wananchi wa mkoa wa Manyara, kuanzia tarehe 20 Januari, 2025 pamoja na Miradi mingine inayotekelezwa na Wakala katika mkoa wa Manyara.
Mhandisi, Advera Mwijage akitoa taarifa kuhusu Mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo 6 ambayo itaanza kusambazwa kwa Wananchi wa mkoa wa Manyara, kuanzia tarehe 20 Januari, 2025 pamoja na Miradi mingine inayotekelezwa na Wakala katika mkoa wa Manyara.
Mhandisi, Advera Mwijage akikabidhim, Mhe. Queen Sendiga, Mkuu wa mkoa wa Manyara, Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia; fomu za maombi ya mkopo nafuu wa ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini pamoja na miongozo ya namna ya kupata fursa hiyo, ofisini kwa Mkuu wa mkoa wa Manyara, leo, tarehe 16 Desemba, 2024.
Mhandisi, Advera Mwijage akifafanua mambo mbalimbali mbele ya Wanahabari (Hawapo pichani) baada ya kukamilika kwa mazungumzo yake na Mkuu wa mkoa wa Manyara.
📌Wananchi 3,255 kila wilaya ya mkoa huo kunufaika
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA); kuanzia tarehe 20 Januari, 2025 itaanza kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 mkoani Manyara ili kusaidia Wananchi kutumia nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.
Hayo yamesemwa leo, tarehe 16 Desemba, 2024 na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, kutoka REA, Mhandisi, Advera Mwijage mbele ya Mhe. Queen Sendika, Mkuu wa mkoa wa Manyara, ofisini kwake, Babati, mkoani humo.
Katika mpango huo; Mkoa wa Manyara unataraji kupokea mitungi ya gesi 16,275 yenye thamani ya shilingi milioni 284 ambayo, itasambazwa kwa Wananchi katika wilaya zote tano huku kampuni ya MANJIS Logistic Ltd ikipewa jukumu la kusambaza mitungi hiyo kwa gharama ya shilingi 17,500 kwa kila mtungi (Bei ya ruzuku).
Imeelezwa kuwa Serikali, itatoa ruzuku ya asilimia 50 kwenye kila mitungi ambapo bei ya awali, ilipaswa kuwa shilingi 35,000 ili kununua mtungi pamoja na kichomeo chake.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amepongeza juhudi hizo za Serikali na kuongeza kuwa lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, jambo ambalo litasaidia kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Serikali, imeweka ruzuku ya asilimia 50, kwa hiyo wakina Baba na kina Mama wa mkoa wa Manyara, wajiandae kutumia gesi, tuwapunguzie wakina Mama kushika masizi, kutumia kuni na mikaa, kwetu sisi Mradi huu ni neema”. Alisema, Mhe. Sendiga.
Kwa upande wake, Mhandisi, Adivera Kaijage amesema kwa nchi nzima Mradi huo wa kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa Wananchi utagharimu shilingi bilioni 8 ambapo kwa mkoa wa Manyara shilingi milioni 284 zitatumika kugharamia mitungi 16,275.
“Kampuni ya MANJIS imeshinda, tenda ya kusambaza mitungi hiyo, ilitangaza ofa ya kusambaza mtungi mmoja kwa shilingi 35,000 kwa kutambua hilo, Serikali italipia asilimia 50 ya bei hiyo, ambayo itakuwa shilingi 17,500.” Alifafanua, Mhandisi, Advera.
Mhandisi, Advera amesema ili kupata mtungi huo wenye ruzuku ya Serikali kila Mwananchi anapaswa kuwa na kitambulisho cha NIDA au namba ya NIDA.
Amesema, REA pia, inaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali, ambapo à metoa taarifa ya Mradi wa mkopo wenye riba nafuu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo ya vijijini huku akisema Watu wengi wamekuwa wakitunza mafuta katika nyumba wanazoishi jambo ambalo ni hatari kiafya pamoja na ubora wa mafuta hayo.
“Tumeona vyombo vya moto vya Watu wa vijijini vitaharibika kwa sababu mafuta wanayotumia ni machafu hayana uhifadhi mzuri, unaohitajika, lakini pia gharama za usafiri maeneo ya vijijini ni kubwa na Wananchi hawanufaiki kwa bei elekezi zinazotolewa na Serikali”. Amesema,Mhandisi, Advera
“Mkopo huo utalipwa ndani ya miaka 7; kwa riba ya asilimia 5; mkopo hauzidi milion 133, kwa ajili ya kujenga kituo ambacho kutakuwa na matenki mawili yenye ujazo wa lita 15,000.
Mhandisi Kaijage pia ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Manyara kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya maombi ya mkopo nafuu wa ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta maeneo ya vijijini.
Mkoa wa Manyara una jumla ya wilaya 5; wilaya hizo ambazo Wananchi wake watanufaika na mitungi ya gesi ni pamoja na wilaya ya Babati, Hanang, Simanjiro, Mbulu na Kiteto.
No comments:
Post a Comment