SERIKALI YASISITIZA UBORA NA USIMAMIZI WA MIRADI SERIKALI ZA MITAA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, December 16, 2024

SERIKALI YASISITIZA UBORA NA USIMAMIZI WA MIRADI SERIKALI ZA MITAA.



Na. Mwandishi Wetu – MAELEZO


Naibu Waziri Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Festo John Dugange amesema Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya kuwanufaisha wananchi ikiwemo ujenzi wa zahanati ,hospitali, shule, vituo vya afya, barabara na huduma za maji mijini na vijiji kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi kwenye bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini.

Dkt. Dugange amesema hayo wakati akifungua kongamano la wadau wa Serikali za mitaa kutoka maeneo mbalimbali nchini leo Desemba 16, 2024 Jijini Dodoma ambapo amesema Serikali imejenga zahanati zaidi ya 1900, vituo vya afya 872 huku asilimia 99 ya Halmashauri zote nchini zikiwa na hospitali.

“Kazi ya serikali za mitaa ni kuharakisha maendeleo yanawafikia wananchi. Serikali tutaendelea kuimàrisha ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, tumefanya uwekezaji mkubwa na kuwekeza rasilimali nyingi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali za Mitaa ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara, mabweni ya wanafunzi na barabara” amesisitiza Dkt. Dugange.

Amesema viongozi wa serikali za mitaa wanalo jukumu la kuwezesha ustawi wa wananchi na kuhakikisha usimamizi mzuri wa rasilimali zinazoelekezwa kwenye maeneo ya Serikali za Mitaa huku akibainisha kuwa kongamano hilo linatoa fursa kwa wadau wa Serikali za mitaa kujadili namna ambavyo Serikali itaendelea kuimarisha na kuboresha ufanisi na utendaji kazi ili kufikia malengo ya kitafa.

Dkt. Dugange amesema viongozi wa serikali za mitaa wana kazi kubwa ya kuibua na kusimamia vyanzo vya mapato katika maeneo yao ili wananchi waone faida na matunda ya uwepo wa Serikali za mitaa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayoanzishwa.

“Tunapaswa kukusanya mapato ya ndani kwa ufanisi, kudhibiti matumizi na kupunguza utegemezi wa Halmashauri zetu kwa Serikali kuu, matarajio ya Serikali ni kuona miradi iliyopangwa hususani ujenzi wa majengo ya Serikali ya kutolea huduma yanakamilika kwa wakati na ubora kwa kuzingatia fedha zilizotengwa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI (Uongozi Institute), Kadari Singo amesema taasisi ya uongozi imekutana na wadau hao ili kutoa mafunzo yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma katika maeneo ya Serikali za Mitaa.

Amesema taasisi ya uongozi itaendelea kuimarisha uelewa na kutoa fursa kwa viongozi wa serikali na wadau mbalimbali kupatiwa mafunzo ili kuongeza ufanisi na utoaji wa huduma kwa wananchi.





No comments:

Post a Comment