TANROADS YAIMARISHA UDHIBITI WA UZITO WA MAGARI KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA NA KUFANYA BARABARA KUDUMU MUDA MREFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, January 17, 2025

TANROADS YAIMARISHA UDHIBITI WA UZITO WA MAGARI KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA NA KUFANYA BARABARA KUDUMU MUDA MREFU



Meneja wa Mizani wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Leonard Mombia ameeleza umuhimu wa kutumia mizani katika kudhibiti uzito wa magari kama njia ya kulinda barabara na miundombinu mingine nchini.

Akizungumza kutoka Makao Makuu ya TANROADS, Mha. Mombia amesisitiza kuwa, udhibiti wa uzito wa magari ni hatua muhimu kwa kuhakikisha barabara zinadumu kwa muda uliopangwa na kuepuka gharama kubwa za matengenezo.

Amesema barabara za lami zinapaswa kudumu kwa angalau miaka 20, huku barabara za zege zikitarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 40.

Hata hivyo, magari yenye uzito wa ziada hupunguza muda huo wa matumizi.

"Barabara inapobeba magari mazito kupita kiasi, umri wake unapungua, na badala ya kudumu miaka 20, inaweza kudumu miaka 15 au chini ya hapo," alifafanua.

Mizani zimefungwa katika barabara nyingi nchini ili kudhibiti uzito wa magari. TANROADS inatumia aina mbalimbali za mizani, ikiwemo ile isiyohamishika, inayohamishika, na ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo.

Mha. Mombia amebainisha kuwa mizani inayopima huku gari likiwa kwenye inasaidia kuchuja magari yenye uzito wa kawaida na kuelekeza yale yenye uzito kupita kiasi kwenye mizani maalum kwa upimaji wa kina.

Taarifa zinazokusanywa kwenye mizani ni muhimu kwa usalama wa barabara na matumizi mengine.

Taarifa hizo ni pamoja na uzito wa gari, dereva, mmiliki wa gari, na mwelekeo wa safari.

"Hii hutusaidia kufuatilia mwenendo wa magari na kutoa msaada kwa taasisi nyingine kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na vyombo vya usalama inapohitajika," alisema Mha. Mombia.

TANROADS inatekeleza udhibiti huu kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayodhibiti uzito, urefu, na upana wa magari. Lengo ni kuzuia ajali na uharibifu wa miundombinu. Mhandisi Leonard alieleza kuwa magari yanayozidisha uzito au madereva wanaokwepa mizani hupigwa faini kulingana na kanuni.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza kwenye mifumo ya kisasa ya mizani, ikiwemo mifumo ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo.

Mhandisi Leonard ameeleza kuwa uwekezaji huu sio tu unarahisisha usafirishaji wa ndani, bali pia unachangia katika biashara ya kikanda, hususan kwa nchi zinazotumia bandari na barabara za Tanzania.

Mha. Mombia amewasihi wasafirishaji kufuata sheria na kutumia mizani kwa usahihi.

"Mizani ni kwa manufaa ya wote, tunapolinda barabara, tunalinda uchumi wa nchi na maisha ya watumiaji wote wa barabara," alisisitiza.

TANROADS inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha barabara na miundombinu inatumika kwa ufanisi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.









No comments:

Post a Comment