JKCI YAHUDUMIA WAGONJWA 745,837 KATIKA MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 26, 2025

JKCI YAHUDUMIA WAGONJWA 745,837 KATIKA MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, akizingumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita leo tarehe 26 Februari, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.


Na Mwandishi Wetu _DODOMA 


Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za afya ya moyo, ikihudumia jumla ya wagonjwa 745,837.


Akitoa taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne ndani ya Taasisi hiyo leo Februari 26,2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema kuwa idadi hiyo ni kielelezo cha mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia uwekezaji wa Serikali na jitihada za wataalamu wa afya nchini.

JKCI imefanikiwa kupanua huduma zake kwa kuanzisha kliniki mpya katika maeneo ya Kawe na Oysterbay, jijini Dar es Salaam. Kliniki hizi zinatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima, pamoja na huduma nyingine za kibingwa.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ya moyo bila vikwazo vya umbali na gharama kubwa,” amesema Dkt. Kisenge.

Katika juhudi za kuhakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi wengi zaidi, JKCI imeanzisha huduma za tiba mkoba zinazoitwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services. Kupitia programu hii, taasisi hiyo imefanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa watu 21,324 katika mikoa 20 nchini.

Dkt. Kisenge ameeleza kuwa wagonjwa 8,873 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu, huku 3,249 wakihitaji matibabu ya kibingwa.


Mbali na huduma za ndani ya nchi, JKCI imepanua huduma zake kwa kuvuka mipaka na kutoa matibabu katika nchi za Malawi, Zambia, na Jamhuri ya Watu wa Comoro. Katika mataifa haya, jumla ya wagonjwa 1,189 walihudumiwa, na kati yao 262 walipewa rufaa ya kuja kutibiwa Tanzania.

“Tunajivunia kuwa JKCI si tu inaokoa maisha ya Watanzania, bali pia inasaidia wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika,” amesisitiza Dkt. Kisenge.

Taasisi hiyo pia imekuwa ikihudumia wagonjwa kutoka nje ya nchi, ambapo katika miaka minne iliyopita, imepokea wagonjwa 689 kutoka mataifa mbalimbali kama Somalia, Kenya, Msumbiji, Nigeria, na hata nchi za Ulaya kama Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza. Hii inathibitisha ubora wa huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo na jinsi ilivyojijengea heshima kimataifa.

Katika eneo la upasuaji wa moyo, JKCI imefanya upasuaji mkubwa wa kufungua kifua kwa wagonjwa 2,784, ambapo mishipa ya damu, valvu za moyo na mapafu zilibadilishwa au kurekebishwa. Pia, wagonjwa 8,789 walifanyiwa uchunguzi na matibabu ya mishipa ya damu ya moyo kwa kutumia mtambo wa Cathlab, ambao ni maabara maalum ya mionzi.

Ili kuhakikisha kuwa huduma zinaboreshwa zaidi, Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 2.16 katika taasisi hiyo. Fedha hizi zimetumika katika upanuzi wa ICU za watoto na watu wazima, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, tiba mtandao, na mafunzo kwa wataalamu wa afya.

“Uwekezaji huu umeongeza uwezo wetu wa kuhudumia wagonjwa wengi zaidi na kwa ubora wa hali ya juu,” amesema Dkt. Kisenge.

Katika sekta ya utafiti na mafunzo, JKCI imeingia makubaliano na vyuo vikuu mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha New York nchini Marekani, na Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha Poland kwa lengo la kuboresha tafiti za magonjwa ya moyo na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya.

Dkt. Kisenge ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika JKCI na kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inapata mahitaji yote muhimu ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Tunaendelea kuboresha huduma na tunajivunia mafanikio tuliyopata. Azma yetu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha matibabu ya moyo barani Afrika,” amesema.

No comments:

Post a Comment