MFUKO WA UTAMADUNI NA SANAA WACHOCHEA MAENDELEO YA WASANII TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 28, 2025

MFUKO WA UTAMADUNI NA SANAA WACHOCHEA MAENDELEO YA WASANII TANZANIA




Na Okuly Julius _DODOMA


Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Bi. Nyakaho Mahemba,amesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita Mfuko huo umetoa mafunzo kwa Wasanii 11,684 katika mikoa 18 ya Tanzania Bara kati ya hao wanawake ni 6985 Sawa na asilimia 59.8 na wanaume 4699 Sawa na asilimia 40.2

Pia amesema Mfuko huo umekuwa daraja la kuchochea uwasilishaji wa kazi za Wasanii ambapo jumla ya Wasanii 8154 wamewasilisha kazi zao katika maeneo mbalimbali

Bi. Mahemba ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita leo tarehe 28 Februari, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma .

Amebainisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanawawezesha wasanii kugeuza Sanaa kutoka kuwa burudani na kuwa biashara ili iweze kuwazalishia kipato kitakachowasaidia kujikimu na kuchangia katika pato la Taifa.

“Mafunzo yanayotolewa yanahusisha mada mbalimbali kama vile uwekaji akiba, umuhimu wa urasimishaji, uandishi wa maandiko ya miradi, Sanaa na afya, biashara na familia na uwekaji wa kumbukumbu wa mapato ya kila siku.

Mtendaji huyo amesema kwa mwaka ujao wa fedha mfuko wa Utamaduni na Sanaa umejipanga kuzidisha ubora na ufanisi wa utoaji wa Huduma kwa walengwa pamoja na kushirikiana na wadau katika kutatua kero na changamoto za walengwa

Amefafanua kuwa katika kutekeleza maelekezo anayoyatoa Rais Dk. Samia mara kwa mara ya kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau hasa walio katika sekta binafsi.

Amesema mfuko umejipanga kuwezesha wasanii wadogo, wachanga na chipukizi kupitia utoaji wa ruzuku ili kuwawezesha kukuza na kuendeleza vipaji vyao na kuwapa nafasi ya kufanya kazi nzuri katika Sanaa na Utamaduni hasa wakati ambapo hawana uwezo wa kifedha wa kufadhili miradi yao.

Katika hatua nyingine Bi. Mahemba amesema serikali ya Awamu ya Sita ilichukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuongeza bajeti ya Mfuko ili uweze kutekeleza majukumu yake ya Msingi.

Vileviele bajeti ya mfuko imeongezeka hadi kufikia sh. bilioni tatu kwa mwaka huu wa fedha kutoka sh. bilioni 1.6 sawa na ongezeko la asilimia 87.5.

“Kupitia uongozi mahiri na madhubuti wa Rais Dk. Samia ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mfuko umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya sh.bilioni 5.2 kwa miradi 359 ya sanaa iliyozalisha jumla ya ajira 497,213,”amesema

Ameongeza kuwa :”Maeneo ya miradi ya iliyowezeshwa ni muziki, filamu , maonesho, Ufundi, Lugha na Fasihi. Mikoa iliyofikiwa ni 18 ambayo ni Dar- Es Salaam, Arusha, Morogoro, Pwani, Geita, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara, Kilimanjaro, Simiyu, Kigoma na Katavi,"

No comments:

Post a Comment