MHE.MCHENGERWA AONYA VIKUNDI HEWA MIKOPO YA 10% - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, February 8, 2025

MHE.MCHENGERWA AONYA VIKUNDI HEWA MIKOPO YA 10%


OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Mohamed Mchengerwa amesema Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa watakaobainika maeneo yao kuwa na vikundi hewa kwenye mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu watawajibishwa.

Aidha, zaidi ya Sh.Bilioni 234 zinakusudiwa kupelekwa kwa wananchi kwa njia mbili za utoaji mikopo hiyo ambazo ni kupitia Benki kwa Halmashauri 10 na mikopo iliyoboreshwa kwenye Halmashauri 174.

Akizungumza Februari 7, 2025 jijini Dodoma kwenye hafla ya utiaji saini mikataba kati ya Halmashauri 10 na Benki tatu ya utoaji mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani, Mhe. Mchengerwa amesema kila mmoja afuatilie fedha hizo kuhakikisha zikishuka kama ilivyokusudiwa kwa walengwa ili zitabadili maisha yao.

Amesisitiza uadilifu wa kwenye fedha hizo na kufuatilia kwa kina vikundi vyote na kuvijua na asisikie vikundi hewa.

“Fedha hizi ni za moto wajibu wetu ni kumsaidia Rais fedha hizi zisiende kuchezewa, naelekeza kikundi hewa kitakachobainika eneo lolote viongozi wa eneo hilo mtapaswa kuwajibika, tumieni vyombo mnavyosimamia kwenye mikoa na wilaya kuhakikisha hakuna vikundi hewa, fedha zisimamiwe na kurejeshwa."


“Nazielekeza Mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kuchangia fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo hii kwa mujibu wa sheria ya fedha za serikali za mitaa, na Katibu Mkuu niletee orodha kama kuna halmashauri ambazo hazijachangia na zinadorora kuchangia na kama kuna halmashauri ambayo haijatekeleza maelekezo ya Rais,”amesema.

Amesema Benki ya NMB itafanya kazi kwenye halmashauri za wilaya za Bumbuli, Itilima, Newala, Manispaa ya Songea, Jiji la Dodoma huku benki ya CRDB itafanya kazi Wilaya za Nkasi, Mji wa Mbulu, Manispaa ya Kigoma na Jiji la Dar es salaam na Benki ya Biashara ya Uchumi itafanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Siha.

Awali, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Adolf Ndunguru amesema kusainiwa mikataba hiyo ni mwanzo wa mapinduzi ya kuhakikisha mikopo hiyo ya asilimia 10 inakuwa na tija tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

No comments:

Post a Comment