MKANDARASI BARABARA YA OMUGAKORONGO - MURONGO KUPATIKANA FEBRUARI, 2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 11, 2025

MKANDARASI BARABARA YA OMUGAKORONGO - MURONGO KUPATIKANA FEBRUARI, 2025


Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema zabuni ya ujenzi wa barabara ya Omugakorongo – Kigarama – Murongo (km 110), sehemu ya Murongo hadi Businde (km 53.4) imetangazwa upya baada ya zabuni ya awali kukosa Makandarasi wenye sifa.

Aidha, Zabuni mpya ilitangazwa mnamo tarehe 6 Oktoba 2024 na kufunguliwa tarehe 12 Desemba 2024 ambapo kazi ya uchambuzi wa zabuni inaendelea na inatarajiwa kukamilika katikati ya mwezi Februari 2025 na baadaye hatua za kumkabidhi Mkandarasi zitaendelea.

Hayo yameelezwa leo Februari 11, 2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kyerwa Innocent Bilakwate aliyeuliza ni lini ujenzi wa barabara ya Omugakorongo - Kigarama hadi Murongo utaanza baada ya barabara hii kutangazwa upya.

“Ni kweli kwamba barabara hii ndio inaunganisha Tanzania na Uganda kupitia Kyerwa na tayari tumeshatangaza kipande cha kwanza ambacho tupo kwenye hatua za mwisho za manunuzi na kwa kipande cha pili tumeshakamilisha usanifu na tunaendelea kutafuta fedha ili tuweze kukamilisha kilometa zote”, amesema Eng. Kasekenya.

Kuhusu Barabara ya Omurushaka - Nkwenda Eng. Kasekenya amesema tayari Mkandarasi ameshalipwa na kwa sasa yupo kwenye hatua za awali (mobilization) na kama kuna changamoto ya kuchelewa kuanza kwa mradi Wizara ifahamishwe ili ihakikishe anasimamiwa na kuanza kazi mara moja.

Vilevile, Wizara ya Ujenzi imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kisorya - Rugezi na barabara unganishi ya Nansio - Rugezi (km 11) ambapo utekelezaji wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara unganishi kutoka Nansio - Rugezi (km 7) umeanza mwezi Februari 2024 na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja.

No comments:

Post a Comment