
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis leo tarehe 25 Februari, 2025 Makongo Juu jijini Dar es Salaam ameungana na viongozi na waombolezaji katika kuifariji familia ya Marehemu Bi. Sifael Mushi, aliyeshiriki tukio la kuchanganya udongo wa Muunganio wa Tanganyika na Zanzibar, ambaye amefariki dunia Februari 20, 2025.
Marehemu Bi. Sifael amefariki dunia katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Akitoa salamu za Serikali mara baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu Bi. Sifael, Naibu Waziri Khamis amesema marehemu amefanya kazi kubwa kwa taifa kwa kuweka historia ya Muungano ambao hadi leo matunda yake yanaonekana.
Mhe. Khamis amesema Marehemu Sifael alikuwa mtu wa watu na mmoja wa watu muhimu katik taifa hili aliyetengeeza historia kubwa ambayo itakwenda kudumu milele hata kizazi kinachokuja kitakwenda kutambua mchango wake.
“Leo hii tunaona Muungano wetu ulivyo imara na unaendelea kudumu na hata wananchi wa pande zote mbili wanashirikiana, wanavuka maji (bahari) kutoka upande mmoja kwenda mwingine yote ni kwasababu ya kazi kubwa aliyoifanya mama huyu,” ameeleza.
Mhe. Naibu Waziri ametumia nafasi hiyo Mhe. kuwasilisha salamu rambirambi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango
Amesema viongozi hao wakuu wapo pamoja na familia ya marehemu na wanatoa pole kwa kumpoteza mtu muhimu katika taifa hili na kwamba ataendelea kukumbukwa na kusomwa katika historia.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema kizazi cha sasa kina mengi ya kutafakari na kujifunza kutokana na maisha ya viongozi walioasisi Muungano ambao unatimiza miaka Zaidi ya 60.
Amemtaja Marehemu Sifael kuwa ni mfano wa kuigwa kwa kazi ya uzalendo na utii aliounesha alipokuwa miongoni mwa Watanzania walioshiriki katika zoezi la kuchanganya udongo wa Muungano.





No comments:
Post a Comment