Prof. Nombo ameeleza hayo Februari 26, 2025 jijini Dodoma akifungua Mkutano wa Pamoja wa Tathimini ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu ambapo amesema nguvu kubwa inahitajika kwenye ujenzi wa miundombinu.
Miundombinu hiyo ni pamoja na madarasa na karakana upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwemo vifaa vya mafunzo ya amali na TEHAMA na Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini.
"Serikali inaendelea na maandalizi ya zana za kuwezesha utekelezaji wa Sera ikiwemo miongozo, nyaraka, mapitio ya Sheria ya elimu na kuweka mifumo mbalimbali." amesema Prof. Nombo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu Msingi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maulid Mnonya amesema Serikali imekuja nampango mkakati wa kuzalisha walimu wa amali ambapo Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo cha Mtwara na Chuo cha Mtwara Ufundi sasa vitakuwa ndani ya Must kwa ajili ya kutoa walimu wa amali.
Akielezea utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mfunzo ya Amali yam waka 2014 toleo la mwaka 2023 na mitaala mipya, amesema Serikali tunajiandaa itakapofika mwaka 2027 kuna watakaokuwa wanamaliza darasa la sita na la saba wote wanahitaji kwenda sekondari tumejiandaa kwa ujenzi wa shule na ajira za walimu na mambo mbalimbali,”amesema.
Maulid amesema baada ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTIVET), kwenda kuzifanyia ukaguzi ili kuona iwapo shule 101, zinakidhi kuanzisha mafunzo ya amali, walibaini kuwa shule 99 ndizo zilikuwa zimekidhi vigezo.
Hata hivyo amesema shule 39, 25 zikiwa za Serikali ndizo walizoona kuwa zinafaa kuanza kwa kuwa lengo la utekelezaji wa mlengo huo ni wa amali.
Amesema katika awamu hiyo ya kwanza wanafunzi 2,000 kati yao 184 wakiwa ni wale wenye mahitaji maalumu waliingia katika mkondo wa elimu mbalimbali.
Amesema jumla ya fani 15 na kati yao fani ndogo ndogo zikiwa ni 75 ziliingia katika awamu ya kwanza na zilizingatia mazingira na mahitaji ya jamii eneo la husika.
Maulid amesema kuwa kulikuwa na upungufu wa walimu wa amali 4633 lakini Serikali imetoa kibali kwa ajili ya kuwaajiri walimu hao.
Aidha, amesema walikuwa wanatakiwa kuanza elimu ya amali kwa kidato cha tano mwaka jana lakini hawakuweza kuanza kutokana na kutofanyika kwa mafunzo ya walimu na kukosekana kwa vitabu.
Hata hivyo, amesema hivyo vyote vipo sasa na kuwa wataanza utekelezaji wa mkondo huo mwaka huu.
Maulid amesema elimu ya amali inaanzia katika shule za msingi katika kilimo na michezo ambapo wanafunzi wanaanza kujengeka huko.
Kuhusu changamoto, Maulid amesema changamoto waliyokutana nayo ni wingi wa wanafunzi baadhi ya madarasa yalikuwa na wanafunzi hadi 80 badala ya 45 kama sera inavyotaka.
Aidha, amesema wanajenga shule 103 na mwaka huu wanaendelea kukamilisha shule 26 za amali ambazo ziko katika mikoa mbalimbali.
“Kwa hiyo shule zinazojengwa zitakuwa full pamoja na vifaa vyake. Vyuo vyetu vyote vitatoa walimu kwa ajili ya shule za msingi, zamani vilikuwa vinatoa walimu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari,”amesema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) Martha Makula ameshauri bajeti ya elimu iongezwe na kufikia asilimia 20 ya bajeti ya kila mwaka na kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vya elimu vinavyoingizwa hapa nchini.
No comments:
Post a Comment