ULEGA AAGIZA UTEKELEZAJI MIRADI SEKTA YA UJENZI KUZINGATIA THAMANI YA FEDHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 13, 2025

ULEGA AAGIZA UTEKELEZAJI MIRADI SEKTA YA UJENZI KUZINGATIA THAMANI YA FEDHA


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameelekeza Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Ujenzi kuhakikisha wanazingatia thamani ya fedha wakati wa utekelezaji na usimamizi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo barabara, madaraja, vivuko, majengo ya Serikali na viwanja vya ndege.

Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyanyakazi wa Sekta hiyo mkoani Singida, Waziri Ulega pamoja na mambo mengine amesisitiza kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za Serikali katika miradi inayosimamiwa.

“Nawaelekeza muendelee kuunga mkono dhamira hii njema ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwenye miradi mnayoisimamia”, amesema Ulega

Aidha, Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuongeza juhudi za usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya dharura ya miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua El-Nino na Kimbunga Hidaya yenye thamani ya Shilingi takriban Bilioni 868.56.

Ameelekeza Viongozi wa Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kuhakikisha kuwa dhana ya uwezeshaji wa Makandarasi wa ndani inatekelezwa kama ilivyokusudiwa ili kunufaisha na kuwajengea uwezo Makandarasi hao.

Amewataka wataalam wa Sekta ya Ujenzi kutumia Mkutano huo kujadili namna ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam kwa kutumia barabara zilizo na Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), ili kupunguza msongamano kwenye njia za magari binafsi.

“Tumieni kikao hiki kutafakari na kujadili namna sahihi ya kutumia barabara hizo ili ziweze kukuza uchumi na kuleta tija kwa watumiaji na serikali kwa kupunguza msongamano nyakati za asubuhi na jioni” amefafanua Ulega.
Amewasisitiza watumishi wa Sekta ya Ujenzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, maarifa na uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kuufungua mkoa wa Singida kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami ambazo zimesaidia kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika mkoa huo.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza hilo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi, Aisha Amour amesema kuwa Wizara inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi na ujenzi wa daraja la Mwendokasi (BRT) jijini Dar es Salaam.

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Ujenzi umefanyika mkoani Singida ambapo ajenda kuu katika Mkutano huo ni kupokea, kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwakawa fedha 2025/26 kabla ya Bajeti hiyo kuwasilishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushirikisha wajumbe mbalimbali kutoka Wizarani na Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.






No comments:

Post a Comment