VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUPIGA VITA RUSHWA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 25, 2025

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUPIGA VITA RUSHWA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025



Na Barnabas Kisengi, Gairo


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Gairo, mkoani Morogoro, imeendesha mafunzo maalum kwa viongozi wa dini kuhusu njia bora za kuzuia na kupambana na rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Gairo, Bi Julieth Mtuy, amesema lengo ni kujenga ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa dini na taasisi hiyo ili kukabiliana na vitendo vya rushwa katika kipindi cha uchaguzi.

"Tumeamua kuanza na viongozi wa dini kwa sababu wana ushawishi mkubwa kwa waumini wao kupitia mahubiri katika makanisa na misikiti. Kupitia wao, elimu hii itawafikia wananchi kwa haraka na kwa ufanisi," amesema Bi Mtuy.

Aidha, amesisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwa nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa ili kuhakikisha Tanzania inasalia kuwa nchi ya amani na wananchi wanajivunia utaifa wao.


Kwa upande wake, Afisa wa TAKUKURU wilaya ya Gairo, Mohamed Kimolo, ameeleza kuhusu nafasi ya viongozi wa dini katika mapambano dhidi ya rushwa, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, na Madiwani.

"Tunakaribia uchaguzi mkuu, na ni wajibu wenu kama viongozi wa dini kuhakikisha mnawakemea wale wanaohusika na vitendo vya rushwa. Tukishirikiana kwa pamoja, tutaweza kuangamiza rushwa nchini," amesisitiza Kimolo.

Mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za TAKUKURU kuhakikisha makundi mbalimbali yanapata elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa kabla ya Uchaguzi Mkuu nchini.

No comments:

Post a Comment