WANANCHI WILAYANI SUMBAWANGA WANUFAIKA NA UJENZI WA MADARAJA NA BARABARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 20, 2025

WANANCHI WILAYANI SUMBAWANGA WANUFAIKA NA UJENZI WA MADARAJA NA BARABARA


Sumbawanga, Rukwa


WANANCHI wa kata za Miangalua na Kasanzama Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa wameishukuru serikali kupitia TARURA kwa kuwajengea madaraja matatu ya mawe katika barabara ya Laela-Kavifuti-Miangalua yanayounganisha kata hizo kwenda Makao Makuu ya wilaya Laela.

Wakizungumza kwa hisia kubwa wananchi hao wamedai kuwa hapo awali walikuwa wakipata shida hasa kipindi cha mvua kutokana na kukosa kivuko cha kupita hali ambayo ilikuwa inapelekea kukosa mawasiliano.

Naye, Bw. William Vicent Afisa Mtendaji wa Kata ya Miangalua ameishukuru serikali kwa kuwajengea madaraja matatu katika barabara hiyo ambapo kulikuwa ni kikwazo kutoka kijiji cha Kavifuti kwenda Makao Makuu ya wilaya Laela kufuata huduma za kijamii.

“Tulishindwa kupata mapato kwasababu barabara hii ilikuwa haipitiki na mazao mengi hayakuweza kuuzwa ndio maana bei ya mazao iliweza kushuka, lakini sasa hivi wananchi watapata fursa nzuri kupeleka mazao yao sokoni na kuuza bei inayofaa”, amesema.

Bw. Emmanuel Sindani mkazi wa kijiji cha Kavifuti amesema, awali mvua ilikuwa ikinyesha njia ya kwenda Laela hakukuwa na mawasiliano, wananchi walikuwa wakipata shida kwenda kituo cha afya lakini sasa wanapita bila shida, wanaishukuru TARURA kwa ujenzi wa madaraja hayo lakini wanaomba kama kuna uwezekano mita 800 zilizobaki wawekewe kalavati nje ya lililopo ili kusitokee shida kipindi cha mvua kubwa njia ipitike muda wote.

Bi. Teddy Clement mkazi wa Kavifuti kipindi cha nyuma tulipata shida kabla ya daraja hapa palikuwa panajaa maji tunashindwa kubeba mazao yetu kutoa shambani kupeleka sokoni sasa hivi tunapita vizuri kwa baiskeli, pikipiki bila shida na kupeleka mazo yetu sokoni.

Kwa upande wake, Mhandisi Rashidi Katema, msimamizi wa mradi kutoka TARURA wilaya ya Sumbawanga amesema, mradi huo umehusisha ujenzi wa daraja la mawe la Kusa mita 19, daraja la mawe la mto Kizembe mita 16 na daraja la mawe la Shikwizya mita 13 katika barabara ya Laela-Kavifuti-Miangalua ambapo utekelezaji wa mradi umekamilika kwa 100%.

Ameongeza kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara chini ya mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.

No comments:

Post a Comment