WASAIDIZI WA MSAADA WA KISHERIA WASISITIZWA KUWA MABALOZI WA AMANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 26, 2025

WASAIDIZI WA MSAADA WA KISHERIA WASISITIZWA KUWA MABALOZI WA AMANI



Na Mwandishi Wetu _DODOMA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula amewasisitiza wasaidizi wa Msaada wa kisheria (yaani Paralegal) kuwa mabalozi wazuri na kutokuwa chanzo cha kusababisha migogoro mbalimbali katika Jamii nchini.

"Kimsingi wana msaada mkubwa Kwa Serikali, na Serikali itaendelea kuwajengea uwezo na pale ambapo patakapokuwa na majengo ya ziada tutawapatia ofisi" amesema.

Dkt. Franklin Rwezimula ameyasema hayo leo Februari 26,2025 jijini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo Maalum ya siku 15 kwa wasaidizi wa Msaada wa kisheria (Paralegal).

Amesema wasaidizi wa Msaada Wa kisheria (Paralegal) wana msaada mkubwa katika jamii kwani hatuna watoa huduma wa msaada wa kisheria wa kutosha hapa nchini, ambao wana degree au wamepita kwenye mafunzo ya madarasani.

"Hawa Wasaidizi wa kisheria wameenea nchi nzima,wanatusaidia na wana mchango mkubwa sana katika jamii" amesema.

Aidha, Dkt. Rwezimula amesema wasaidizi hao watawasajili kwenye mfumo wao maalum ili waweze kufanya kazi vile ipasavyo, na wale ambao wataenda ndivyo sivyo wataondolewa kwenye mfumo huo.

"Uzoefu unaonesha wengi wanafanya vizuri, kwahiyo hii itatusaidia kuongeza watoa msaada wa kisheria wengi zaidi hasa kwenye maeneo ya pembezoni ambapo hakuna mashirika mengi lakini kuna makundi maalum hasa wakina mama na watoto" amesema Dkt. Rwezimula

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility (LSF),Bw. Amani Manyelezi, amesema mfuko huo umekuwa ukiunga mkono msaada wa kisheria kwa zaidi ya miaka 12 kwa kushirikiana na mashirika 184 na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 3,000 nchini.

"Tunalenga kuweka mazingira wezeshi kwa wasaidizi wa kisheria kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, huku tukizingatia usawa wa kijinsia na kupambana na ukatili wa kijinsia, hasa dhidi ya wanawake na watoto," amesema Bw.Manyelezi.

Hata hivyo amefafanua kuwa kila mwaka wasaidizi wa kisheria wanawafikia zaidi ya wananchi milioni 6, wengi wao wakiwa wa maeneo ya vijijini ambako huduma za msaada wa kisheria ni adimu.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 59 ya kesi zinazowasilishwa kwa wasaidizi wa kisheria hutolewa na wanawake, huku asilimia 41 zikihusisha wanaume. Kesi nyingi zinahusiana na masuala ya ndoa na mgawanyo wa mali.

Naye Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria, Laurent Burilo-Mwakilfehi, amesema licha ya kuwepo kwa wasaidizi wa kisheria 2,205 waliosajiliwa, bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu hao, hususan vijijini.

"Huduma ya msaada wa kisheria ni bure, hivyo tunawasihi wasaidizi wa kisheria kufanya kazi kwa uzalendo na moyo wa kujitoa. Hii ni kazi ya kiuchungaji, malipo yake ni kuona haki inatendeka kwa jamii," amesema Burilo-Mwakilfehi.

Mafunzo hayo yatadumu kwa muda wa miezi miwili na nusu, ikiwa ni sehemu ya programu ya miezi mitatu ya mafunzo kwa vitendo, kabla ya wahitimu kupatiwa vyeti rasmi na kusajiliwa kama wasaidizi wa kisheria.





No comments:

Post a Comment