
Na Okuly Julius _DODOMA
WAZIRI wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi amekemea tabia ya baadhi ya watangazaji kubananga Kiswahili kwani inaondoa maana halisi ya baadhi ya maneno na kupotosha jamii.
Ameyasema hayo leo Februari 13 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa vyombo vya Utangazaji Nchini, iliyoongozwa na kauli mbiu isemayo "wajibu wa vyombo vya Utangazaji kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025"
Amesema kuwa kumezuka tabia kwenye jamii ya kutumia maneno ya kiswahili ambayo yamekuwa yakipotosha maana halisi.
"Tunabananga kiswahili matokeo yake majirani zetu wanasema watanzania hawaongei lugha fasaha na sio mahiri kwenye kiswahili na Wabanangaji wakubwa wa kiswahili ni watangazaji," amesema
Amesema kuwa Watangazaji wakongwe walitumia kamusi na walipokuwa na wasiwasi walipiga simu ili kujua neno hilo ni sahihi au sio sahihi.
Amesema kuwa watangazaji wa redio na televisheni wana jukumu kubwa la kuhakikisha Watanzania wanaongea kiswahili sahihi.
Pia amewataka wadau kubadilishana mawazo, uzoefu na fursa zilizopo katika tasnia hiyo nchini
"Mabadiliko ya tabia nchi ni ajenda ya kitaifa, kwani yamekuwa yakihusika moja kwa moja katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, na kumekuwa na tahadhari kwenye misimu ya mvua na joto duniani.
"Redio imekuwa ni chombo muhimu cha kutoa taarifa kwa wananchi ni muhimu taaluma ya utangazaji ikazingatiwa," amesema
Profesa Kabudi ameongeza kuwa taaluma ya utangazaji nchini imekuwa ikitumika kuleta umoja kwa taifa, serikali nyingi duniani imekuwa ikitumia vyombo vya habari, kwa ajili ya kufikisha taarifa sahihi.
"Serikali zilizopo madarani zimekuwa zikitumia vyombo hivyo kama nyenzo ya utulivu na kuhamasisha amani, mshikamano," amesema
Amesema sekta ya habari imekumbwa na mabadiliko ya teknioloijia na serikali inapitia changamoto mbalimbali na iliagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya uchambuzi wa sekta ya utangazaji na ripoti rasmi itawasilishwa Februari mwaka huu.
Matokeo ya kazi hiyo yataleta chachu mpya ya kuboresha vyombo vya utangazaji nchini ili kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya habari, sanaa na michezo.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amewataka wadau kuzingatia weledi, nidhamu katika tasnia ya utangazaji.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Jabir Bakari amesema mamlaka hiyo imejiwekea utaratibu wa kukutana na vyombo vya habari angalau mara moja kwa mwaka kwa lengo la kushauriana, kutafuta suluhu ya changamoto na kurekebishana.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Saida Mukhi amewataka wadau wa utangazaji kuepuka kutengeneza maudhui yanayokiuka maadili ya utangazaji nchini na kuwa tayari kufanyia kazi nasaha zilizotolewa na viongozi
"kuweni makini mnavyotumia Akili Unde kwa sababu kuna baadhi maudhui yanaweza kupotosha hivyo ni vyema kujiridhisha sio kila kitu unachokipata kwa kutumia Akili Unde ukipeleke hewani moja kwa moja," amesisitiza Mukhi






No comments:
Post a Comment