MRADI WA SHILINGI BILIONI 10 KUBORESHA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI KWA TEHAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 14, 2025

MRADI WA SHILINGI BILIONI 10 KUBORESHA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI KWA TEHAMA




Na Mwandishi Wetu, DODOMA


KIASI cha Shilingi bilioni 10 kinatarajiwa kutumika kutekeleza mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi nchini.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, alisema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuzindua mradi huo.

Prof. Mushi alisema mradi huo, ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu, utaboresha mazingira ya walimu kutumia TEHAMA kufundisha kwa ufanisi na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi nchini.

“Mradi huu wa miaka mitatu utagharimu kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 4, sawa na Shilingi bilioni 10 za Kitanzania, ikiwa ni ufadhili kutoka Korea. Utajikita katika maeneo manne muhimu ya maendeleo ya TEHAMA kwenye elimu,” alisema Prof. Mushi.

Aidha, alisema kupitia mradi huo, Taasisi ya Elimu nchini itaandaa mitaala na kuiweka katika mfumo wa kidijitali ili kutoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kutoka maeneo mbalimbali kwa kutumia TEHAMA.

“Pia, kazi nyingine ni kutengeneza mfumo wa kupima weledi wa wanafunzi katika matumizi ya TEHAMA, kuongeza ushawishi wa kisera, na kuhakikisha kuna sera zitakazosaidia kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji,” aliongeza.

Vile vile, alisema mradi huo utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maarifa ya TEHAMA kwa wanafunzi waliopo vijijini kutokana na uwiano mdogo wa walimu waliopo nchini.

“Mradi huu unakuja wakati mwafaka ambapo tayari tumezindua sera mpya ya elimu ya mwaka 2023, inayosisitiza matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji,” alisema.

Naibu Balozi wa Korea nchini Tanzania, Lee Seungyun, alisema mradi huo utasaidia vijana wa Kitanzania kuongeza ujuzi katika TEHAMA na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa kutumia teknolojia hiyo.

Naye, Mratibu wa mradi huo, Lina Rujweka, alisema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa wizara mbalimbali, ikiwemo Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania.





No comments:

Post a Comment