
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF umetoa semina kwa wafanyakazi wa TAEC kuhusu huduma zinazotolewa na mfuko huo ikiwa ni Pamoja na kuwakumbusha wanachama mafao yatokanayo na michango wanayokatwa kila mwezi.
Akizungumza Jijini Dodoma katika ofisi za Makao Makuu ya TAEC Afisa Mafao Mkuu PSSSF Kanda ya Kati Bwn. Ramadhani Sossora amesema mafao yatolewayo na mfuko huo ni pamoja na mafao ya muda mrefu na mafao ya muda mfupi. Mafao ya muda mrefu ni; Mafao ya Uzeeni, Mafao ya Ulemavu, Mafao ya Kifo na Mafao ya Wategemezi. Kwa upande wa mafao ya muda mfupi ni; Mafao ya Kukosa Ajira, Mafao ya Ugonjwa na Mafao ya Uzazi.
Kuhusu Mafao ya Uzazi. Mafao haya hutolewa kwa mwanamke mwanachama ambaye amechangia miezi 36 au zaidi,
Madai yafunguliwe na nyaraka zote ziwe zimewasilishwa ndani ya siku 90 baada ya kujifungua, mwanachama atalipwa mshahara mmoja, hata hivyo kiwango hakitozidi shilingi milioni moja.
Mafao ya Uzeeni: Umri wa kustaafu kwa hiari wa miaka 55 na kwa lazima miaka 60.
Pensheni ya Uzeeni inawahusu pia Wanachama walioko kwenye Utumishi wa Umma ambao ajira zao zinasimamiwa na sheria mahsusi ambazo zinaelekeza umri wa kustaafu kulingana na taaluma na kada walizopo mathalan Jeshi la Polisi na Magereza, Madakatari Bingwa, Waadhiri Waandamizi na Majaji.
Sifa ya mwanachama awe amechangia kwenye Mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi 180 au miaka 15.
Mafao ya kifo: Mtumishi akifariki akiwa kazini ni fao la kifo masharti yake ni Pamoja na Iwapo Mwanachama aliyefariki hakuchangia miezi 180, wategemezi watalipwa mkupuo maalum (special lumpsum), hakutakuwa na pensheni ya kila mwezi.
Mafao ya wategemezi: ni kwa mwanachama atakayefariki akiwa na miezi zaidi ya 180 ya uchangiaji, kiinua mgongo kitagawanywa kwa warithi kama ambavyo mahakama itaelekeza kwenye nyaraka ya mgao, pia mwenza na watoto watalipwa pensheni ya kila mwezi.
Ikiwa kuna mtoto mwenye zaidi ya miaka 21 mwenye ulemavu wa mwili au akili atalipwa penesheni kwa maisha yake yote.
Mafao ya kukosa ajira: Mwanachama awe amechangia kipindi cha miezi 18 lakini kisichozidi miezi 180.
Kwa Mwanachama aliyechangia chini ya miezi 18 atalipwa nusu ya michango yake
Awe ameachishwa kazi kwa mujibu wa taratibu (termination) au kumalizika kwa mkataba, isipokuwa kuacha kazi kwa hiari (resignation),
Mafao ya Ugonjwa: Awe anaumwa au amepata ajali ambayo haijatokana na kazi yake na atalipwa asilimia arobaini (40%) ya mshahara aliokuwa akipata kabla ya ugonjwa au ajali. Mafao haya yatalipwa kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu.
Awe hajatimiza umri wa kustaafu kwa hiari
Awe amechangia kwa kipindi cha miezi 36, ambapo miezi 12 kati ya hiyo iwe imelipwa ndani ya mwaka mmoja kabla ya ugonjwa.
Fao la ulemavu: Mafao haya hulipwa kwa Mwanachama aliyeachishwa kazi baada ya kupoteza uwezo wake wa kufanya kazi kutokana na maradhi, ulemavu wa mwili au akili kama itakavyothibitishwa na jopo la madakatari
Awe na ulemavu au maradhi ambayo hayajatokana na ajira yake (wanaopoteza uweza wa kufanya kazi kutokana na ajali au maradhi yatakanayo na ajira zao hulipwa chini ya mpango wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Mafao haya hulipwa kwa sehemu mbili, ambazo ni malipo ya mkupuo na pensheni ya mwezi kwa kipindi chote cha uhai wa mwanachama iwapo amechangia kipindi cha miezi isiyopungua miezi thelathini na sita (36) na kati ya hiyo, miezi kumi na mbili (12) ya mwisho iwe na michango.
Aidha Bwn. Sossora amesema PSSSF imeongeza asilimia 2 ya pensheni kwa wanachama wake wote kuanzia Januari Mosi 2025, Pia Mstaafu ambaye anapata pensheni ya PSSSF akifariki mfuko utatoa shilingi laki tano kusaidia gharama za mazishi Pamoja na kulipa mtegemezi miezi 36 ya pensheni aliyokuwa anapata mstaafu.
Sambamba na hayo Bwn. Sossora amesema hakuna ucheleweshaji wa wastaafu kupata mafao yao na mtumishi akistaafu hulipwa ndani ya siku 60 .





No comments:
Post a Comment