Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wakala wa barabara za vijijini (TARURA) imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofanyika kwa kutumia teknolojia mbadala wakianza na barabara ya Chamwino na kuhitimisha ziara hiyo katika daraja la Ng’ong’ona linaloonganisha barabara ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na wananchi waishio kata ya Ng’ong’ona.
Akizungumza leo Machi 12, 2024 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa bodi ya ushauri TARURA Mhandisi Florian Kabaka amesema ujenzi huo umetumia teknolojia mpya hivyo ni muhimu kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa lengo la kuona kama zinafaa kwa matumizi ya watanzania au lah.
“Mbali na gharama ambazo moja kwa moja tumeelezwa na wataalam kwamba ni nafuu sana na kwa ujenzi wa barabara unafuu hauwezi kuupata mwanzo kwasababu gharama za kuanzia zipo juu lakini kwa maana ya muda wake wa maisha yake yote ukionganisha gharama za utengenezaji, ujenzi na kila kitu gharama zinakuwa chini”,
“Upande wa daraja la mawe ni moja kwa moja gharama zina anzia chini na nusu ya gharama ambazo zingejenga daraja lengine kwa njia ya kawaida ambayo tumeizoea, lakini kwa maisha ni yale yale kwa muda ule ule”. amesema Kabaka.
Amesema TARURA imeanza ujenzi wa barabara (Echo Roads) kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kwa upande wa barabara ya Chamwino ambayo ina muda wa miezi saba tangu ujenzi ufanyike, kupitia ziara hiyo wameweza kufanya ukaguzi kujua kama teknolojia hiyo inafaa kwa matumizi ya ujenzi wa barabara.
Aidha Mha. Kabaka ametoa maelekezo kwa TARURA kusimamia vyema miundombinu inayojengwa kwa kuhakikisha inatumia kanuni za ujenzi kikamilifu.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA mkoa wa Dodoma Mha. Edward Lemelo amesema ujenzi wa barabara Km 6.95 ya Chamwino imetumia kemikali ya Echo Roads ambayo imechanganywa katika udongo ili kubeba uzito wa barabara.
“Tumekuja pia katika daraja hili la Ng’ong’ona linaloonganisha chuo cha UDOM na kata ya Ng’ong’ona kwaio wanafunzi, walimu wengi wanatumia daraja hili katika kupita”, amesema Lemelo.
Daraja hilo lenye urefu wa mita 26.4 na upana wa mita 7 lililojengwa kwa mawe, limegharimu kiasi cha Tsh Milioni 152 huku madaraja 8 yakiendelea na ujenzi na 9 kukamilika na kutumiwa na wananchi wa Dodoma.
Aidha Mha. Lemelo ametoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kutunza miundombinu hiyo ya barabara kwa manufaa yao wenyewe.
Sambamba na hayo mkazi wa kata ya Ng’ong’onda Rose Lusano ameishukuru TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limepunguza changamoto waliokuwa wakipata awali ikiwemo kuzunguka umbali mrefu na kupita katika matope.
Nae Charles Mpili ambaye ni mzaliwa wa Chamwino amesema kupitia TARURA barabara zinaendelea kuboreshwa na kupitia ujenzi wa barabara ya Chamwino umezidi kuchochea maendeleo kutofautisha na miaka ya nyuma
No comments:
Post a Comment