Katika kuelekea Sikukuu ya Eid El Fitr, ambayo huadhimishwa duniani kote baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jeshi la Polisi nchini limejipanga kikamilifu katika mikoa yote kuhakikisha waumini wa dini ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla wanasherehekea kwa amani na utulivu.
Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi katika nyumba za ibada na maeneo yote yenye mikusanyiko mikubwa ya watu. Aidha, wamiliki wa kumbi za starehe wanakumbushwa kuzingatia maelekezo ya kiusalama na taratibu walizopewa wakati wa kupatiwa vibali vya kuendesha shughuli zao.
Wananchi wote wanahimizwa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao na mali zao, kama vile:
- Kuacha nyumba bila uangalizi.
- Kunywa pombe kupita kiasi.
- Kuruhusu watoto au vijana walioko chini ya uangalizi wa wazazi kwenda kwenye kumbi za starehe au maeneo hatarishi kwa usalama na utu wao.
Pia, madereva wanakumbushwa kufuata sheria za usalama barabarani kwa kuepuka:
- Kuendesha wakiwa wamelewa.
- Kupita mwendo kasi.
- Kujaza abiria kupita kiasi.
No comments:
Post a Comment