🎈🎈Bei ya tangawizi yapaa.
Kilosa, Morogoro
Wananchi wa kata ya Lumbiji wilayani Kilosa mkoani Morogoro wameishukuru Serikali kupitia TARURA kuwajengea barabara ya Ludewa - Lumbiji yenye urefu wa Km 21.6.
Wananchi hao wanaojishughulisha na Kilimo cha mazao ya chakula na biashara wamefurahia ujenzi wa barabara hiyo kwani imerahisisha kusafirisha mazao kwenda sokoni kwa urahisi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kisongwe, Bw. Festo Sekaila amesema kuwa barabara hiyo ilikuwa imeharibika hadi kupelekea kupata hasara ya mazao yao kutokana na gharama ya usafirishaji kuwa juu.
"Gharama ya kusafirisha gunia moja la mazao ilikuwa kati ya shilingi 30,000 - 35,000, lakini baada ya barabara kutengenezwa gharama ya kusafirisha gunia moja imeshuka mpaka kati ya shilingi 10,000 - 12,000", amebainisha.
Naye, Laurian Mkuchu ameeleza kuwa barabara hiyo ni chanzo cha mapato yanayotokana na kilimo cha mazao mbalimbali kama vile tangawizi, mihogo, mbaazi, viazi na maharage lakini changamoto kubwa ilikuwa ni namna ya kuyasafirisha mazao yao ambapo barabara hiyo imekuja wakati muafaka kwa wanakijiji wa Kisongwe na kata ya Lumbiji kwa jumla.
Akielezea manufaa waliyoanza kuyapata kutokana na ujenzi wa barabara hiyo, Bw. Mchuku amesema kuwa kwa sasa wao kama wakulima hususani wa zao la tangawizi wanaona kama maajabu kwani bei ya tangawizi imepanda kutoka bei ya kati ya shilingi 400 - 500 kwa kilo moja ya tangawizi hadi shilingi 2500 - 3000 .
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa, Mhandisi Juliana Masalo amesema kuwa kata ya Lumbiji ni eneo ambalo lina kilimo kikubwa cha tangawizi na mboga mboga zikiwemo nyanya, nyanya chungu na pilipili lakini barabara hiyo ilikuwa haipitiki kutokana na eneo hilo kuwa na milima na mabonde ya maji yaani 'Swamp area'.
Ameongeza kuwa barabara hiyo imetekelezwa chini ya mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara chini ya mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
No comments:
Post a Comment