Wanawake wa AQRB Waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Jijini Dodoma - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 8, 2025

Wanawake wa AQRB Waadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Jijini Dodoma



Na Okuly Julius, Dodoma


Wanawake wa Bodi ya Wataalamu wa Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) wameungana na wanawake wote duniani kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake leo Machi 8, 2025 .

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkadiriaji Majenzi QS. Shangwe Kambaga ametoa wito kwa wanawake na wasichana kujikita katika masomo ya sayansi na uhandisi kuanzia ngazi za awali, akisisitiza kuwa sekta ya ujenzi bado inahitaji mchango mkubwa wa wanawake.

"Kuhusu usawa wa kijinsia, ni muhimu wanawake watambue kuwa hata kazi ngumu za ujenzi wa miundombinu wanaweza kuzifanya kwa ufanisi. Hamsini kwa hamsini inafanikiwa kwa kushiriki katika kila sekta," amesema QS. Shangwe.

Ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wanawake kwenye sekta ya ujenzi imeongezeka, akitolea mfano uteuzi wa Balozi Aisha Amour kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, jambo linaloonyesha kuwa wanawake wanaweza kuongoza na kutekeleza majukumu makubwa kwa mafanikio.

Kwa upande wake, Hamida Juma, ambaye ni mtumishi wa AQRB, amesisitiza kuwa maadhimisho haya yanawahamasisha wanawake na wasichana kushiriki katika fursa mbalimbali bila kujibagua, kwani wana uwezo wa kufanikisha mambo makubwa wakiwa na msaada au bila msaada.

Sherehe hizi zinaendelea kutoa motisha kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta zote za maendeleo, hususan zile zinazohitaji wataalamu wa sayansi, uhandisi, na ujenzi.


No comments:

Post a Comment