WANAWAKE WA DUWASA WAWASAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM MKOKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 10, 2025

WANAWAKE WA DUWASA WAWASAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM MKOKA




Na Okuly Julius _ DODOMA


Wanawake Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) wameendeleza utamaduni wao wa kila mwaka wa kusaidia watu wenye mahitaji maalum baada ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Leo, Machi 10, 2025, wanawake hao wametembelea Shule ya Msingi Mkoka, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, ambayo ina kituo cha watoto wenye mahitaji maalum, na kutoa misaada yenye thamani ya Shilingi milioni 1.5.

DUWASA YADUMISHA UTAMADUNI WA KUWASAIDIA WENYE MAHITAJI MAALUM

Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo, Katibu wa Wanawake DUWASA, Ester Mlewa, alisema utamaduni huo unalenga kuwafanya wahitaji wajisikie kuwa sehemu muhimu ya jamii.

“Mwaka jana tulitembelea Gereza la Isanga na kuwalipia faini wanawake watatu waliokuwa wamefungwa kwa kushindwa kulipa faini. Pia tulitembelea kituo cha kulelea wazee kilichopo Buigiri na kutoa misaada mbalimbali. Huu wa leo ni mwendelezo wa matendo ya huruma kwa wahitaji,” alisema Mlewa.

Aliongeza kuwa msaada waliotoa unajumuisha madaftari, kalamu, vyakula, nguo, taulo za kike, na mahitaji mengine muhimu. Pia aliwataka taasisi na watu binafsi kujitoa kusaidia wenye ulemavu, kwani msaada huo unaleta faraja na kujenga moyo wa ukarimu kwa watoto.

CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI SHULE YA MKOKA

Mwalimu wa kitengo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule hiyo, Furaha Mwashilindi, alieleza kuwa shule ina jumla ya wanafunzi 122 wenye ulemavu wa ngozi, kusikia, na viungo, huku zaidi ya 80 wakiishi katika hosteli shuleni hapo.

Alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa wahudumu wa watoto wa kike na wa kiume, kwani hakuna waliopo walioajiriwa na serikali. “Shule inalazimika kutafuta wahudumu, lakini wengi huondoka kazi inapokuwa ngumu, hivyo kuwaachia walimu mzigo wa kulea watoto,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa shule inakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kufundishia, hususan kwa watoto wenye ulemavu wa kusikia, ambao wanategemea zaidi mafunzo ya kuona. Alisema shule inahitaji projekta ili kuboresha ufundishaji kwa watoto hao.

Mwalimu Mwashilindi aliishukuru serikali kwa kuwajengea uzio shuleni hapo, hatua ambayo imesaidia kuwalinda watoto wenye ulemavu wa akili dhidi ya kutoroka. Pia aliiomba serikali kujenga hosteli mpya kwa ajili ya watoto wa kike, kwani iliyopo sasa haina miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu.

WATOTO WAISHUKURU DUWASA

Baadhi ya watoto waliopokea msaada huo waliishukuru DUWASA kwa kuwakumbuka na kuwapatia mahitaji muhimu. Walitoa wito kwa watu wengine kusaidia vituo vya watoto wenye mahitaji maalum, wakisema msaada huo unaleta faraja kubwa kwao.







No comments:

Post a Comment