Na Okuly Julius _ DODOMA
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Crispin Chalamila, amesema Rushwa katika uchaguzi ni sumu inayoharibu misingi ya demokrasia na utawala bora, na inapotokea huathiri uchaguzi kwa njia mbalimbali, kuvuruga usawa na kutoa upendeleo kwa watu fulani.
Akifungua warsha leo Aprili 10,2025 jijini Dodoma kwa viongozi wa taasisi zinazohusika na uchaguzi,Chalamila amesema warsha hiyo inalenga kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia rushwa wakati wa uchaguzi.
Taasisi hizo zina jukumu la kusimamia sheria, kutoa elimu ya uraia, kufuatilia matumizi ya fedha zinazotumiwa na vyama vya siasa na wagombea, kuchunguza na kuendesha mashtaka, pamoja na kuhakikisha uwajibikaji katika kila hatua ya uchaguzi.
“Hili ni jambo muhimu katika kukuza demokrasia na utawala bora, kulinda usalama na kuchochea maendeleo ya nchi,” alisema.
Ameongeza kuwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi ni moja ya vikwazo vya kutokuwa na uchaguzi unaozingatia misingi ya haki na usawa, na vinavyoathiri haki na fursa ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
“Ni kwa sababu hii, kwa pamoja tunapaswa kuchukua hatua na kuweka mikakati ya kuzuia vitendo vya rushwa katika mchakato wa uchaguzi, na ndiyo maana tumekutana hapa ili tujadili na tujipange pamoja,” alieleza.
Amesema warsha hiyo imeandaliwa kwa kutambua kuwa uchaguzi huru na wa haki hauwezi kuwepo bila ushiriki wa pamoja wa taasisi za serikali, kila moja ikitimiza wajibu wake kikamilifu na kwa mujibu wa sheria, weledi, uwazi na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
“TAKUKURU inaamini kuwa kwa kushirikiana baina ya taasisi hizi na kuchukua hatua stahiki kwa haraka, ndipo mafanikio katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi yatapatikana,” alisema.
Pia, ameeleza kuwa rushwa hudhoofisha utawala bora na demokrasia kwa kuwanyima wananchi wenye sifa za uongozi nafasi ya kugombea au kuchaguliwa, hali inayosababisha kuchaguliwa kwa viongozi wala rushwa wasioweza kuongoza kwa misingi ya haki, ambayo ndiyo msingi wa ustawi wa wananchi.
Aidha, ameongeza kuwa rushwa husababisha uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara, na kuifanya nchi kugubikwa na vitendo vya rushwa vinavyosababisha baadhi ya wananchi kupoteza imani na mifumo ya taasisi na serikali, na hatimaye kuchangia machafuko.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa watumishi wa umma na taasisi za serikali zinazoshiriki katika mchakato wa uchaguzi kuhakikisha kwamba wanapanga na kutekeleza mikakati ya kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.
Ameeleza kuwa ili kuzuia vitendo hivyo, taasisi hizo zina wajibu wa kuhakikisha uteuzi wa wagombea unazingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na usawa wa fursa, kuzuia matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kudhibiti fedha za kampeni na kuhakikisha upatikanaji sawa wa fursa kwa vyama vya siasa na wagombea.
Vilevile, kuhakikisha mazingira salama na ya haki bila vitisho wakati wa kupiga kura, na kuhakikisha ushughulikiaji wa malalamiko unafanyika kwa uwazi na haki, pamoja na kuchukua hatua dhidi ya watumishi na wanasiasa waliokiuka maadili.
Amesema warsha hiyo pia imelenga kujenga uelewa wa viashiria vya rushwa vinavyoambatana na uchaguzi, kubadilishana uzoefu na mbinu bora za kukabiliana na tatizo hilo wakati wa uchaguzi, na kuweka misingi ya ushirikiano baina ya taasisi hizo.
Ameeleza kuwa mada zitakazojadiliwa ni pamoja na namna ya kutambua mianya ya rushwa katika uchaguzi, na namna ya kudhibiti vitendo vya rushwa kabla na baada ya uchaguzi.
Kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2025 unakuwa huru na wa haki, alibainisha kuwa serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuanzisha Tume Huru ya Uchaguzi, kutunga Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, kuimarisha TAKUKURU, pamoja na kuboresha sheria kwa kuweka kifungu cha adhabu kwa watakaobainika kujihusisha na rushwa wakati wa uchaguzi.
No comments:
Post a Comment