SERIKALI YAWATAKA WAZAZI KUSHAURIANA NA WATOTO KABLA YA KUFANYA MABADILIKO YA TAHASUSI NA KOZI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 2, 2025

SERIKALI YAWATAKA WAZAZI KUSHAURIANA NA WATOTO KABLA YA KUFANYA MABADILIKO YA TAHASUSI NA KOZI



Na Okuly Julius_ DODOMA


Serikali imewataka wazazi kushauriana na watoto wao kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalam na kitaaluma, kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au kozi bila kuwalazimisha juu ya kufanya mabadiliko ya tahasusi za kusoma Kidato cha Tano na kozi za vyuo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2024 kufanya mabadiliko ya tahasusi za Kidato cha Tano na kozi za vyuo kwa njia ya mtandao kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kidato cha Tano na Vyuo mwaka 2025.

Mchengerwa amesema kuwa zoezi la kubadilisha tahasusi na vyuo lilianza rasmi tarehe 31 Machi 2025 na litakamilika tarehe 30 Aprili 2025.

"Wanafunzi, wazazi, na walezi wanakumbushwa kushauriana kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalam na kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au kozi," alisema Mchengerwa.

Aliongeza kuwa, "Ninawasisitiza wanafunzi, wazazi, na walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo kutangazwa. Ni muhimu kuzingatia muda uliotolewa wa kufanya marekebisho ili ratiba ya kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo iweze kuendelea kwa muda uliopangwa. Baada ya matokeo ya kujiunga na Kidato cha Tano na vyuo kutangazwa, ofisi haitashughulikia changamoto hizo kwa kuwa fursa ya kufanya mabadiliko hayo imeshatolewa," alisema Waziri Mchengerwa.

Amesema kuwa serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye Fomu za Uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni.

Waziri Mchengerwa pia amesisitiza kuwa huduma hiyo ya kubadilisha tahasusi ni bure, na iwapo wanafunzi watakumbana na changamoto, wanapaswa kuwasiliana na Dawati la Huduma kwa Mteja kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kupiga simu kwa namba +255 262 160 210 na +255 735 160 210.

Itakumbukwa kuwa serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya tahasusi (combination) na kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi (Selform). Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

No comments:

Post a Comment