
🎈🎈Serikali yatumia jukwaa la kimataifa kutangaza fursa za uwekezaji, utalii na biashara
Na Okuly Julius _ DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na TANTRADE, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – SMZ, imethibitisha ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Dunia (Expo 2025 Osaka) yatakayofanyika kuanzia Aprili 12 hadi Oktoba 13, 2025, katika Kisiwa cha Yumeshima, Osaka, Japan.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Aprili 8,2025 jijini Dodoma Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt.Selemani Jafo amesema Expo 2025 Osaka, yenye kaulimbiu kuu “Kuwezesha jamii kwa Maisha Endelevu”, inalenga kuunganisha mataifa duniani kutafuta suluhu za changamoto za kisasa.
Ambapo Tanzania imechagua kauli mbiu ndogo ya “Kuunganisha Maisha – Connecting Lives” ikiwa na dhamira ya kuunganisha uzalishaji wa ndani na masoko ya kimataifa, kukuza uwekezaji, biashara na miundombinu ya kisasa.
Dkt.Jafo amesema matarajio na Malengo
Katika Expo hiyo ni kuvutia zaidi ya watembeleaji milioni 28, Tanzania inalenga kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na utalii; kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi; na kuitangaza nchi kimataifa kupitia mila, desturi na utamaduni wake.
"Banda la Tanzania litakuwa na ukubwa wa mita za mraba 53 na eneo la biashara la mita 15, na litatumika kuonyesha miradi ya kimkakati inayovutia wawekezaji na watalii kutoka pande zote za dunia,"
Na kuongeza kuwa "Tanzania ina historia ndefu ya ushiriki katika maonesho ya EXPO tangu mwaka 1967. Katika Expo 2020 Dubai, Tanzania ilifanikiwa kupata mikataba 36 ya makubaliano yenye thamani ya dola bilioni 8 (Shilingi trilioni 18.5) na kutembelewa na watu 928,469, hatua iliyowezesha kampuni za Tanzania kutangaza bidhaa na huduma kwa mafanikio makubwa,"ameeleza Dkt.Jafo
Amesema Expo 2025 Osaka itakuwa na programu nane maalum zitakazofanyika kwa nyakati tofauti, zikiangazia sekta za utalii, afya, miundombinu, nishati, kilimo, teknolojia, na uwezeshaji wanawake.
Aidha, Mei 25, 2025 imetengwa kuwa Siku ya Tanzania ambapo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na siku hiyo itatumiwa kuonesha vivutio vya Tanzania na kuhamasisha ushirikiano wa kibiashara.
"Siku inayofuata, Mei 26, Tanzania itaandaa Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii ambalo litaweka jukwaa la majadiliano ya kina kati ya wadau wa ndani na makampuni ya kimataifa kutoka Japan na mataifa mengine," amesema Dkt.Jafo
Pia serikali imetoa wito kwa taasisi za umma, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maandalizi na utekelezaji wa shughuli za Expo hiyo kwa kuwasilisha maudhui ya miradi ya kimkakati, kuthibitisha ushiriki wa kongamano na programu, na kuandaa Mikataba ya Ushirikiano (MoUs) na taasisi za Kijapani.
Usajili kwa ajili ya ushiriki unafanyika kupitia tovuti ya TANTRADE:https://tradefair.tantrade.go.tz/expo2025/expo_registration
"Kwa pamoja, sekta zote za umma na binafsi zinapaswa kutumia Expo 2025 Osaka kama jukwaa muhimu la kuimarisha uchumi wa taifa kupitia biashara, teknolojia, utalii, uwekezaji na diplomasia.Tanzania yajipanga kung’ara kimataifa – Tushirikiane kuimarisha uchumi wetu," amesisitiza Dkt.Jafo
No comments:
Post a Comment