Na Mwandishi Wetu, Makete - Njombe
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imepongezwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kujenga mazingira wezeshi kwa sekta binafsi nchini iliyowezesha wananchi waliopo maeneo ya Vijijini na pembezoni mwa miji kupata huduma bora ya nishati ya umeme kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Pongezi hizo zimetolewa leo na TEF mara baada ya kutembelea mradi wa umeme wa Ijangala (Ijangala Mini Hydropower Plant 360 kW) uliopo Wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Mwenyekiti wa TEF, Bw. Deodatus Balile ameipongeza REA kwa kuweka kiasi kikubwa cha fedha takribani shilingi bilioni 2 za kuendeleza na kutekeleza mradi huo ambao umesaidia kuongeza ubora na upatikanaji wa umeme mkoa wa Njombe.
"Sisi TEF tumejionea kwa macho yetu kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kupitia REA kwenye mradi huu mkubwa. Nimeambiwa ipo miradi mingine ambayo pia inapewa ruzuku na Serikali ikiwemo mradi wa Luponde, Lugarawa, Ikondo Matembwe na Ludilu, hongereni sana REA, " Amesema Bw. Balile.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya amesema Wakala umekuwa ukifadhili miradi ya uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme vijijini hususani inayotekelezwa na taasisi mbalimbali za Serikali na za watu binafsi kwa kutoa ruzuku pamoja na mikopo ya masharti nafuu.
"Ruzuku hisi zinawezesha utekelezaji wa miradi hiyo sambamba na uwezeshaji wa fedha na elimu ya kuwajengea uwezo waendelezaji hawa imekuwa ikitolewa pia, " Amesema Mha. Yessaya.
Amesema kuwa, mradi wa Ijangala umeleta faida mbalimbali ikiwemo kuongezeka kiwango cha umeme unaozalishwa nchini, kuimarisha hali ya ubora wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na kusaidia kupunguza hewa ya ukaa ambayo ingezalishwa kwa kutumia vyanzo vingine vya umeme.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Umeme Ijangala, Daudi Sanga amesema kwa kiasi kikubwa mradi huo umefadhiliwa na REA na wadau wengine wa maendeleo na mradi huo wa Ijangala kwa sasa unazalisha kilowati 360 zinazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.











No comments:
Post a Comment