
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Wakala wa Vipimo (WMA) umeahidi kuimarisha ushirikiano na Maafisa Biashara wa Mikoa nchini katika kuhakikisha shughuli za biashara zinaendeshwa kwa kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi, huku haki na maslahi ya mlaji yakilindwa.
Ahadi hiyo imetolewa na Meneja wa Sehemu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa WMA, Jadi Athumani Kijumu, Agosti 17,2026 jijini Dodoma, wakati wa Mkutano wa Tatu wa Maafisa Biashara wa Mikoa ulioandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Kijumu amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa Maafisa Biashara wana nafasi kubwa ya kuwa kiungo kati ya WMA, wafanyabiashara na Serikali za Mikoa, hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya udhibiti wa vipimo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema WMA imetumia mkutano huo kutoa elimu kwa Maafisa Biashara kuhusu majukumu ya Wakala, pamoja na namna wanavyoweza kushirikiana katika kutatua changamoto zinazohusu matumizi ya vipimo na kulinda haki za watumiaji.
“Maafisa Biashara ni kiungo muhimu kati yetu na wafanyabiashara waliopo katika mikoa. Ushirikiano wao utatusaidia kuwafahamu wafanyabiashara na maeneo wanayofanyia biashara ili kurahisisha huduma za ukaguzi na ufuatiliaji,” amesema.
Aidha, amesema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha utendaji wa Kamati za Ushauri za Mikoa, ambazo pande zote mbili ni wajumbe, kwa kuwezesha kero na malalamiko ya wafanyabiashara kushughulikiwa kwa wakati.
Kwa upande wa ulinzi wa mlaji, WMA imewataka Maafisa Biashara kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia vipimo vilivyokaguliwa na kuthibitishwa kuwa sahihi, huku wakizingatia pia masuala ya afya na usalama katika utoaji wa huduma na uuzaji wa bidhaa.
WMA pia imesisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali ili kuwezesha ukaguzi na ufuatiliaji kufanyika kwa ufanisi.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za biashara, kupunguza malalamiko yanayotokana na matumizi ya vipimo visivyo sahihi na kuongeza uaminifu kati ya wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa na huduma nchini.




No comments:
Post a Comment