
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Miradi mikubwa miwili ya kimkakati inayotekelezwa katika Jiji la Dodoma ikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na Barabara ya Mzunguko ya Nje ya Jiji (Ring Road) imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wake huku ikiendelea kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza Oktoba 10, 2025 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, amesema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato umefikia asilimia 96.95 kwa upande wa miundombinu na asilimia 63 kwa upande wa majengo, huku thamani ya utekelezaji wa jumla ikiwa shilingi bilioni 360.
Mhandisi Zuhura amesema uwanja huo, ambao unajengwa kwa daraja la 4E, utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba hadi abiria 350.
Uwanja huo unatarajiwa kukamilika Februari 21, 2026 kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi.
“Tunafuatilia kwa karibu kuhakikisha viwango vya ujenzi vilivyowekwa vinazingatiwa na kazi inakamilika kwa ubora unaotakiwa ili kupata thamani halisi ya fedha zilizotumika,” alisema Mhandisi Zuhura.
Aidha, ujenzi wa majengo muhimu unaendelea, ikiwemo jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka, jengo la mnara wa kuongozea ndege (Control Tower) lenye urefu wa mita 56, majengo ya kufua umeme, kituo cha zimamoto, na jengo la hali ya hewa.

Kwa upande wa miundombinu, ujenzi unahusisha barabara ya kutua na kuruka ndege yenye urefu wa kilomita 3.6, barabara za viungio, eneo la maegesho ya ndege, na barabara kuu ya kuunganisha kutoka Arusha hadi uwanjani yenye urefu wa kilomita 5.6 na eneo la maegesho ya magari litakuwa na uwezo wa kuhifadhi hadi magari 500.
Kwa upande mwingine, mradi wa Barabara ya Mzunguko wa Nje ya Jiji la Dodoma (Ring Road) umefikia asilimia 91 ya utekelezaji kwa thamani ya shilingi bilioni 221.7, na unatarajiwa kukamilika Desemba 29, 2025.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 112.3 inagusa maeneo ya Nala, Veyula, Mtumba, Matumbulu na kurudi Nala, ikilenga kupunguza msongamano katikati ya jiji. Ujenzi huo unahusisha barabara za kiwango cha lami, madaraja makubwa, makaravati, njia za watembea kwa miguu, na uwekaji wa taa za barabarani.
Mhandisi Zuhura amesema mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa wananchi, ikiwemo ajira zaidi ya 1,000 kwa wakazi wa Dodoma na maeneo jirani, pamoja na fursa kwa kampuni za ndani kusambaza vifaa vya ujenzi kama nondo, saruji na mafuta.
“Mradi huu utapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katikati ya jiji, kwani magari kutoka mikoa ya jirani kama Singida, Arusha au Iringa hayatalazimika kuingia katikati ya Dodoma,” alieleza.
Mbali na ujenzi wa barabara, TANROADS inatekeleza miradi ambatishi ya kijani na kijamii, ikiwemo upandaji wa miti zaidi ya laki moja na nusu (150,000) pembezoni mwa barabara ili kuhifadhi mazingira, miradi ya umwagiliaji kwa njia ya drip, na uchimbaji wa visima.
Pia, kupitia mpango wa kijamii, ujenzi wa shule ya Chilonwa iliyopo Ihumwa, vituo vinne vya afya, na visima vinne vya maji unaendelea, lengo likiwa ni kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi kandokando ya mradi huo.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza kwenye miradi hii ya kimkakati. TANROADS tutaendelea kusimamia ubora na kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati,” amesema Mhandisi Zuhura.
Miradi hii miwili ya Uwanja wa Ndege wa Msalato na Ring Road Dodoma inatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa mji mkuu wa Tanzania kwa kukuza biashara, utalii na uwekezaji wa kimataifa, sambamba na kuboresha mazingira ya maisha kwa wakazi wa Dodoma.







No comments:
Post a Comment