RUWASA, WADAU WAJADILI UANZISHWAJI VITUO VYA KIUFUNDI HUDUMA YA MAJI VIJIJINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 14, 2026

RUWASA, WADAU WAJADILI UANZISHWAJI VITUO VYA KIUFUNDI HUDUMA YA MAJI VIJIJINI

 


Wadau mbalimbali wa sekta ndogo ya maji vijijini wamekutana Agosti 14, 2026 Jijini Dodoma kwenye warsha ya kujadili mapendekezo ya mpango wa kuboresha huduma za kiufundi kwa kujenga vituo mikoani ili huduma ya maji vijijini inayotolewa kwa Vyombo vya Utoaji Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) iwe endelevu. 


Warsha hiyo iliandaliwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kupitia Kurugenzi ya Huduma za Kiufundi na kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo CBWSOs, na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na miradi ya maji vijijini.


Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya RUWASA Mha. Ngusa Mpembe alisema mpango huo ni muhimu katika kuifanya huduma ya maji vijijini iwe endelevu na kwamba msaada wa kiufundi na vifaa mahsusi vitakavyotolewa katika vituo hivyo vya huduma viainishwe ili kuwe na ufanisi. 

Baadhi Mameneja wa RUWASA wa mikoa na wilaya walipendekeza vituo hivyo vya msaada wa kiufundi vitumie wataalamu wa RUWASA waliopo kwenye ngazi za mikoa na wilaya ili kutoleta mkanganyiko wa kimajukumu. 

 

Akifunga warsha hiyo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Titus Mkapa alisema mpango wa uanzishwaji wa vituo vya huduma za kiufundi katika mikoa 25 kwa ajili ya kuzisaidia CBWSOs unapaswa kutekelezwa vyema ili uweze kufikia lengo la kuhakikisha wananchi wanapa huduma bora na safi za maji kwa wakati kwa uhakika.


Awali akihitimisha majadiliano kuhusu mpango huo, Mkurugenzi wa Huduma za Kiufundi wa RUWASA Mha. Aziz Mutabuzi alisema mpango huo utatekelezwa kwa mtindo wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu na kwamba utashirikisha sekta binafsi katika kuhakikisha huduma ya majisafi inakuwa endelevu.

Naye mwezeshaji katika warsha hiyo Mha. Davis Rweyemamu kutoka RUWASA Makao Makuu alisema wataweka utaratibu wa kuangalia vifaa vitakavyokuwa vinapatikana katika vituo hivyo pamoja na wataalamu watakaoweza kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini unazidi kuimarika na kuwa endelevu.


Nao baadhi ya wadau walioshiriki warsha hiyo walipendekeza uanzishwaji wa vituo hivyo unapaswa kuzingatia madhumuni ya kuanzishwa ili kupunguza gharama za uendeshaji.


Pia walishauri utaratibu wa ununuzi wa vifaa vitakavyohifadhiwa katika vituo hivyo unapaswa kupitia katika mifumo rasmi wa utoaji risiti za kielektroniki pamoja na akaunti maalum zilizoidhinishwa na mamlaka husika.












No comments:

Post a Comment