
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amewasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.
Ripoti hiyo inahusu ukaguzi wa hesabu za serikali kuu, serikali za mitaa, miradi ya maendeleo,mashirika ya umma na ukaguzi wa ufanisi katika maeneo mbalimbali ya matumizi ya fedha za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kichere amewasisitiza kusoma ripoti hiyo ili kuelewa jinsi fedha za umma zinavyotumika .
MASHIRIKA YA UMMA YANAYOTUMIA MIONGOZO YA UTENDAJI KAZI ISIYOJITOSHELEZA
Katika ukaguzi uliofanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024 ulibaini kuwa mashirika ya umma 39 kati ya 217 hayakuwa na miongozo ya utendaji kazi inayojitosheleza kuwezesha mashirika hayo kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Mashirika hayo yalikosa miongozo ya utendaji kazi ikiwemo mipango kazi ya kila mwaka, mifumo ya kisheria ya uanzishwaji na uendeshaji wa mashirika, miongozo ya uhasibu iliyohuishwa na inayoendana na wakati, sera, kanuni za kifedha na sera za usimamizi wa vihatarishi .
Hii ilisababishwa na mapitio na tathmini ya muda mrefu inayofanywa na menejimenti na mamlaka za kuidhinisha.
hivyo, ilibainika kuwepo kwa utegemezi ulipolitiliza wa kimiongozo wa kampuni tanzu kutoka kwa kampuni mama.
Kutokuwepo kwa miongozo ya utendaji kazi katika uendeshaji wa mashirika kuna sababisha changamoto kubwa na kuathiri uwezo wa mashirika katika kufanya kazi kwa ufanisi, kwa uwiano na kwa mujibu wa viwango na kanuni zilizowekwa.
MAAFISA 190 WAMEKAIMU NAFASI ZAIDI YA MIEZI SITA
CAG amebaini mashirika 11 yalikuwa na wafanyakazi 190 waliokuwa kwenye nafasi za kukaimu kwa kipindi kirefu.
Katika ukaguzi huo amebaini wafanyakazi wanaokaimu ambapo mashirika 19 yalikuwa na wafanyakazi 135 waliokuwa wakikaimu nafasi kwa zaidi ya miezi sita, ambapo muda uliozidi kwa kipindi cha miezi sita ulikuwa kati ya mwezi mmoja hadi miezi 57.
Hii ni kinyume na Agizo D.24 (3) la Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma ambalo linataka watumishi wasikaimu nafasi kwa muda usiozidi miezi sita.
USIMAMIZI HAFIFU WA UDHIBITI WA TAKA NGUMU
CAG amebaini kuwa usimamizi hafifu katika Hifadhi za Taifa Lengo C-6-4 la Mpango Mkakati wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa wa mwaka 2022 hadi 2026 linataka asilimia 100 ya aina zote za taka zinazoingizwa na watalii au zinazozalishwa zinakusanywa na kutupwa ipasavyo kwenye maeneo yaliyoidhinishwa huku ikiwa ni takwa la kila mwaka.
Amebaini kuwa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi zilipanga kukusanya taka ngumu za kilo 3,264, hata hivyo, zilikusanya kilo 1,512 hali hiyo ilitokana na usimamizi hafifu wa mpango wa udhibiti taka ngumu, na ufinyu wa bajeti.
Hivyo mwaka wa fedha 2023/24 bajeti ya Mamlaka ya usimamizi na ukusanyaji wa taka ngumu ilikuwa sh. milioni 18.36 na kiasi kilichopokelewa ni shilingi milioni 10.77 na kiasi ambacho hakikutolewa ni shilingi milioni 7.59 sawa na asilimia 41.
Usimamizi duni wa taka ngumu katika Hifadhi za Taifa unachangia upotevu wa bayoanuwai, uharibifu wa mfumo wa ikolojia, na kuenea kwa magonjwa miongoni mwa wanyamapori.
"Ninapendekeza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa iweke mpango wa kina wa usimamizi wa taka ngumu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya usimamizi wa taka ngumu ndani Hifadhi za Taifa,"
No comments:
Post a Comment