BUNGE LAIDHINISHA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 291 KWA WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI MWAKA WA FEDHA 2025/2026 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 16, 2025

BUNGE LAIDHINISHA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 291 KWA WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI MWAKA WA FEDHA 2025/2026



Na Okuly Julius _ DODOMA


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeidhinisha jumla ya Shilingi 291,533,139,000 kwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kutekeleza majukumu na vipaumbele vyake.

Waziri wa wizara hiyo Mhe.Jerry Slaa amesema Kati ya fedha hizo Shilingi 14,485,656,000 zitatumika kwa matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi 6,958,609,000 ni kwa ajili ya mishahara (PE) na Shilingi 7,527,047,000 ni kwa matumizi mengineyo (OC).

Amesema Shilingi 277,047,483,000 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo Shilingi 98,480,905,000 ni fedha za ndani na Shilingi 178,566,578,000 ni fedha za nje.

Aidha Waziri Slaa amesema
kwa upande wa makusanyo ya maduhuli, Wizara hiyo inatarajia kukusanya Shilingi 100,369,242,000 kutokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Katika hotuba hiyo, Waziri Silaa pia ametangaza hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, ikiwemo ujenzi wa Chuo cha Tehama – Digital Technology Institute mkoani Dodoma kitakachozalisha wataalamu wa kudhibiti uhalifu wa kimtandao.

Ameeleza pia kuwa Serikali imebaini na kuzifungia laini za simu 47,728 pamoja na namba 39,028 za Vitambulisho vya Taifa (NIDA) zilizohusishwa na uhalifu wa kimtandao, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda usalama wa sekta ya mawasiliano na kupambana na matumizi mabaya ya teknolojia.

“Sambamba na hilo,” alisema, “Serikali kupitia mamlaka husika, imefanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mikongo ya mawasiliano (fibers) na miundombinu ya watoa huduma katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha ufanisi na usalama wa huduma hizo.”

Pia, Serikali inaendelea kuhuisha mfumo wa takwimu za makosa ya mtandao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uwezo wa udhibiti na ufuatiliaji wa uhalifu huo.









No comments:

Post a Comment