
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema Serikali imebaini na kuzifungia laini za simu 47,728 pamoja na namba 39,028 za Vitambulisho vya Taifa (NIDA) baada ya kugundulika zimehusika katika matukio ya uhalifu wa kimtandao na udanganyifu kwa njia ya mawasiliano.
Hayo yameelezwa leo Mei 16, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni Jijini Dodoma.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha usalama wa sekta ya mawasiliano na kudhibiti matumizi mabaya ya teknolojia, hasa kwa kutumia majina ya watu wengine au vielelezo feki kutenda uhalifu.
“Sambamba na hilo, Serikali kupitia mamlaka husika, imefanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mikongo ya mawasiliano (fibers) na miundombinu ya watoa huduma katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar, kwa lengo la kuhakikisha ufanisi na usalama wa huduma za mawasiliano,” amesema Waziri Silaa


No comments:
Post a Comment