MHANDISI SAMAMBA AHIMIZA UAMINIFU KWA WATOA HUDUMA MIGODINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 16, 2025

MHANDISI SAMAMBA AHIMIZA UAMINIFU KWA WATOA HUDUMA MIGODINI



KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kutokana na utulivu uliopo katika Sekta ya Madini, amekishauri Chama cha Watoa Huduma Sekta ya Madini (TAMISA), kujipanga ili kudhibiti wanachama wake wasio waaminifu katika utoaji huduma.

Mhandisi Samamba ametoa rai hiyo leo jijini Dar es Salaam akizindua Kamati ya Masoko na Mawasiliano ya TAMISA ambapo amesema kitendo cha kuwa na amani na utulivu kwenye Sekta ya Madini ni mafanikio makubwa, hivyo watumie utulivu huo kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini.

“Sekta ya Madini inahitaji mtaji mkubwa, mtu anapokuwa ameweka fedha yake halafu wewe unakuwa sio muaminifu kwenye kazi yake kama Serikali hatutakuvumilia,” ameonya Mhandisi Samamba na kuitaka TAMISA kuwa na meno makali kama ilivyo Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ambayo imekuwa ikiwashughulikia wanachama wake wanaoharibu kazi na Serikali kupitia Wizara ya Madini itatoa ushirikiano kwa asilimia 100, lengo likiwa ni kuleta nidhamu kwenye utoaji wa huduma bora katika Sekta ya Madini.

Naye Kamishna wa Tume ya Madini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content), Dkt. Theresia Numbi amesema mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka 2017, yalipelekea kutungwa kwa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini za Mwaka 2018 ili kutoa tafsiri na kuweka usimamizi thabiti katika utekelezaji wa masuala yote ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini nchini.

Dkt. Numbi amesema pamoja na mambo mengine, Serikali ina jukumu la kuandaa na kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali zenye lengo la kuongeza ushirikiano wa Sekta ya Madini na Sekta nyingine za uchumi ikiwemo kuyataka makampuni ya madini kununua bidhaa na huduma zinazopatikana ndani ya nchi na huduma kutolewa na watanzania.

“Usimamizi wa utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini umepelekea kuibua na kuchochea ongezeko la fursa mbalimbali katika nafasi za ajira na mafunzo; uhaulishaji wa teknolojia; utafiti na maendeleo; pamoja na matumizi ya huduma na bidhaa zinazotolewa na kuzalishwa na Watanzania. Suala hili limepelekea Sekta ya Madini kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya watanzania kwa kuwa fursa nyingi zinatolewa kwa watanzania na kuwapa nafasi ya kukua kiuchumi na kiteknolojia,”amesema Dkt.Numbi.

Amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini itaendelea kusimamia Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini na kuhakikisha kuwa, kipaumbele kinatolewa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na huduma zinazotolewa na watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini, CPA. Venance Kasiki amesema ni wakati sahihi kwa wazawa kushirikiana pamoja na TAMISA kuchangamkia fursa katika shughuli za madini zilizopo katika soko la ndani.

Amesema, hatua hiyo itawapa wazawa nafasi ya kutumia maarifa yao ndani ya mfumo rasmi wa biashara ya madini ili kufikia maendeleo jumuishi.

Kasiki amesema, ushirikiano huo utawezesha uanzishwaji wa miundombinu bora na huduma za kisasa zitakazosaidia wachimbaji wadogo kufikia viwango vya kimataifa.

“ Hii itaongeza ushindani wa bidhaa za ndani na kuleta tija katika sekta kwa ujumla, sambamba na kuongeza mapato kwa taifa na ajira kwa wananchi,’’ amesema CPA Kasiki.

Naye Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalila amesema matarajio yao ni kuona takwimu za Shilingi Trilioni 3.1 zinazotajwa kama fursa kwa wazawa ‘local content’ kwa watoa huduma migodini zinaakisiwa moja kwa moja na watanzania wote na kupitia TAMISA watahakikisha wanachama wao wananufaika na fursa hizo.

Amesema, watafanya mchujo wa kina wa mara kwa mara kwa wanachama wao ili waweze kuaminika na kuepuka kuharibu kazi wanazopata migodini.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano iliyozinduliwa leo, Dkt. Sebastian Ndege amesema, kutokana na Tanzania kuwa na aina mbalimbali za madini na kampuni za nje na ndani ya nchi kuwekeza, ni wakati wa watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.

Amesema, wanafahamu kuwa wanayo haki ya kushiriki katika kutoa huduma lakini pia wanao wajibu wa kuhakikisha wanatoa huduma sahihi kwa wakati sahihi na weledi.

“Sisi kama TAMISA kazi yetu itakuwa ni kusimamia wanachama wetu kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa weledi na kuhakikisha kuwa tunafuata maadili ya utoaji huduma ili tuweze kuaminika na hili tutalisimamia kwa nguvu zetu zote,” amesema Dkt Ndege.













No comments:

Post a Comment