NCAA YASHIRIKI WARSHA YA KUHAMASISHA UANZISHWAJI WA JIOPAKI KATIKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 13, 2025

NCAA YASHIRIKI WARSHA YA KUHAMASISHA UANZISHWAJI WA JIOPAKI KATIKA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI.



Na Mwandishi wetu, Addis Ababa, Ethiopia


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inashiriki warsha ya kimataifa iliyolenga kuhamasisha uanzishwaji wa hifadhi za jiolojia (UNESCO Global Geoparks) katika nchi za Afrika Mashariki iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii ya Ethiopia.

Warsha hiyo inayofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia kuanzia tarehe 12 hadi 15 Mei, 2025 imewakutanisha wataalamu wa Jiolojia, urithi wa asili, malikale na watunga sera kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki ambazo ni Ethiopia, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Djibouti, kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya kuanzisha na kukuza hifadhi za jiolojia katika ukanda wa nchi za Afrika.

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo, Waziri wa Utalii wa Ethiopia, Bi. Selamawit Kassa, alieleza dhamira ya serikali yake kuanza hatua za awali za kuanzisha jiopaki nchini humo, kutokana na urithi mkubwa wa jiolojia uliopo nchini Ethiopia na kusisitiza kuwa jiopaki ni njia muhimu ya kuhifadhi urithi wa asili na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia utalii endelevu.

Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni hifadhi pekee katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara yenye hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai (Ngorongoro Lengai UNESCO Geopark) kupitia kwa Afisa Uhifadhi Mkuu Dkt. Agness Gidna imewasilisha uzoefu na mafanikio yake katika kuanzisha, kusimamia na kuendeleza Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai ambayo ni jiopaki pekee iliyopo kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili barani Afrika ikitanguliwa na M’Goun UNESCO Global Geopark ya Morocco.

Akitoa uzoefu wa usimamizi wa Jiopaki ya Ngorongoro Dkt. Agness Gidna ambae ni mtaalam wa Urithi wa Utamaduni NCAA, alieleza wajumbe wa mkutano huo kuwa hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro Lengai upekee wake unatokana na urithi wa kijiolojia, kiikolojia na kiutamaduni unaojumuisha Mlima Lengai wenye volkano hai ya kipekee duniani na eneo la Ngorongoro lenye historia ya binadamu wa kale pamoja na vivutio vya utalii vilivyopo na jinsi unavyosaidia jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.

Kwa mujibu wa UNESCO, hadi sasa kuna UNESCO Global Geoparks 229 katika nchi 50 duniani, Geopark mbili tu kati ya hizo ndio zilizopo Afrika.

Hali hii inatoa fursa kubwa kwa bara hili kuwekeza zaidi katika kutambua, kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya urithi wa jiolojia, ambayo mengi bado hayajatambuliwa kikamilifu.

Katika warsha hiyo, washiriki wanatarajiwa kuibua mikakati ya pamoja ya kitaifa na kikanda, pamoja na kuanzisha mitandao ya ushirikiano katika kukuza jiopaki kama njia ya kuhifadhi mazingira, kuendeleza elimu, kuimarisha uchumi wa jamii na kuboresha utalii barani Afrika.

Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ilitambuliwa na UNESCO kupata hadhi ya Jiopaaki mwaka 2018 imepata fursa ya kuhamasisha nchi nyingine kufuata nyayo zake katika uanzishaji wa hifadhi za jiolojia, ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa na kinara wa uhifadhi endelevu barani Afrika.


No comments:

Post a Comment