SERIKALI INAITHAMINI SEKTA BINAFSI - WAZIRI MKUU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 13, 2025

SERIKALI INAITHAMINI SEKTA BINAFSI - WAZIRI MKUU




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya kazi kwa karibu sana na sekta binafsi ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Mei 12, 2025) wakati akishiriki mjadala uliojumuisha mawaziri wakuu wanne kutoka Tanzania, Ivory Coast, Guinea na Cameroun katika moja ya vikao vya jukwaa la siku mbili la Maafisa Watendaji Wakuu barani Afrika ambao unaendelea hoteli ya Sofitel jijini Abidjan, Ivory Coast.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jukwaa hilo alitumia fursa hiyo kuelezea namna ambavyo Serikali ya Tanzania imekuwa ikiishirikisha sekta binafsi kwa kufungua milango ya fursa mbalimbali ili iweze kutumika na kuleta manufaa katika nchi.

“Serikali ya Tanzania inafanya kazi kwa karibu na Tanzania Private Sector Foundation, vyama vya wafanyakazi, vya waajiri na wenye viwanda na pia inawapa fursa ya kujenga mshikamano kwa kufanya kazi na Serikali. Pia imefungua milango kwa wawekezaji kutoka ndani ya nchi, nje ya bara la Afrika na duniani kwa ujumla ili kukuza uchumi wa ndani.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza faida za African Continental Free Trade Area (AfCFTA) na jinsi ambavyo Tanzania imetumia fursa hiyo kuimarisha miundombinu ya reli na bandari kutokana na nafasi yake kijiografia. “Tumeimarisha bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara na pia tuna mpango wa kuanza ujenzi wa bandari ya Bagamoyo,” alisema.

Amesema Tanzania inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ili kuziunganisha nchi za Congo, Rwanda na Burundi, pia kuna reli ya TAZARA inayokwenda Zambia. Tumeimarisha usafiri wa anga na barabara ili kuwawezesha wanaokuja kuwekeza Tanzania wapate urahisi wa huduma muhimu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Cosato Chumi alisema kwenye jukwaa hilo limetoa fursa ya kuithibitishia dunia azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza diplomasia ya uchumi na kuifungua Tanzania kiuchumi.

“Washiriki wengi hapa wanaelezea mafanikio ya mkutano mkubwa uliofanyika Januari, 2025 wa Energy Summit, na mikutano mingine mikubwa ambayo nchi yetu imeiandaa. Pia tumepata taarifa kuwa Burkina Faso wanataka kuja nchini kujifunza kuhusu uendeshaji wa hospitali ya Jakaya Kikwete ili nao waweze kujenga hospitali kama hiyo.”

Naye Balozi wa Tanzania nchini Nigeria ambaye ni mwakilishi wa Tanzania nchini Ivory Coast, elestine Kakele amesema ushiriki wa Tanzania kwenye jukwaa hilo unasaidia kutangaza fursa ambazo Tanzania inazo na hasa kwenye zao la mkonge. “Hii ni nafasi muafaka kwa sekta binafsi kuchukua nafasi yake kama injini ya kusukuma maendeleo.”

Naye Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu alisema uwepo wa Tanzania kwenye jukwaa hilo umetoa nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa maendeleo barani Afrika na hivyo kutoa fursa kwa nchi kujitangaza ili kuvutia uwekezaji ambao utawezesha kuiinua nchi kiuchumi.

“Tunaamini kwenye vikao hivi wameendelea kuijua Tanzania na fursa zake zilizoko kwenye uwanda wetu wa logistics, katika madini, kilimo na hata katika sekta ya fedha.”





No comments:

Post a Comment