SERIKALI YA AWAMU YA SITA YATEKELEZA MIRADI YA ZAIDI YA SH. TRILIONI 1.8 SEKTA YA ELIMU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 27, 2025

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YATEKELEZA MIRADI YA ZAIDI YA SH. TRILIONI 1.8 SEKTA YA ELIMU




NA Okuly Julius , Dodoma

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi mikubwa ya kimkakati yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.8 katika sekta ya elimu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu, kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu bora, na kuimarisha ubora wa walimu nchini.

Miradi hiyo imejumuisha ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, mabweni, maabara, nyumba za walimu, na madarasa zaidi ya 8,000 kupitia Mradi wa BOOST. Aidha, serikali imeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kusambaza vifaa vya TEHAMA, kompyuta, na vitabu vya kiada katika shule mbalimbali.

Akizungumza jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa mafanikio hayo yamepatikana kupitia fedha za ndani na zile zilizotolewa na wadau wa maendeleo kupitia mpango wa UVIKO-19.

Katika hatua nyingine, Serikali imeongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka Sh bilioni 570 hadi zaidi ya Sh bilioni 731 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa elimu ya juu kwa vijana wengi zaidi wa Kitanzania.

Pia, vyuo vya ufundi (VETA) na FDC vimeendelea kujengwa katika mikoa na wilaya mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuimarisha elimu ya ufundi na kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi wa kati kwa maendeleo ya taifa.

Katika upande wa tafiti na ubunifu, Serikali kupitia COSTECH na Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) imeendeleza uwekezaji katika tafiti za kisayansi na teknolojia, pamoja na kutoa tuzo na ufadhili kwa wabunifu chipukizi kupitia programu ya Samia Scholarship.

Waziri Mkenda amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni ishara ya dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa jumuishi, bora na endelevu kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.

No comments:

Post a Comment