
Na Okuly Julius , Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema Wizara hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati yenye lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia nchini, ikiwemo ujenzi wa madarasa 12,000, mabweni, na nyumba za walimu, pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA shuleni.
Profesa Mkenda ameyasema hayo leo Mei 27,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Elimu.
"kutekelezwa miradi hiyo imewezesha kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, kuongeza ufaulu, na kuleta usawa katika upatikanaji wa elimu, hasa katika maeneo ya vijijini," ameeleza Profesa Mkenda
Aidha, Profesa Mkenda amesema Serikali kupitia Wizara hiyo, imesambaza vifaa vya TEHAMA kwenye shule zaidi ya 800 na kutoa mafunzo kwa walimu 4,000 ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji wa kisasa.
Hata hivyo,Profesa Mkenda amekiri bado kuna changamoto kadhaa zinaikabili sekta hiyo zikiwemo uhaba wa walimu, vifaa vya kujifunzia, na upungufu wa umeme katika baadhi ya shule, hali inayozorotesha juhudi za kukuza elimu jumuishi na ya kisasa.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeweka mikakati ya kuajiri walimu wapya 12,000, kujenga madarasa mapya 8,000, kusambaza umeme wa jua kwa shule zisizo na nishati ya uhakika, na kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kugharamia na kusimamia miradi ya elimu.
Hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora, jumuishi, na inayokidhi mahitaji ya karne ya 21.
No comments:
Post a Comment