SERIKALI YASAJILI WATATUZI 498 WA MIGOGORO KWA NJIA MBADALA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 20, 2025

SERIKALI YASAJILI WATATUZI 498 WA MIGOGORO KWA NJIA MBADALA




Na Okuly Julius DODOMA


Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imethibitisha kuwa hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya Watatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala 498 wamesajiliwa nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza upatikanaji wa haki kwa gharama nafuu na kwa wakati.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Kwa mujibu wa Waziri Ndumbaro, kati ya watatuzi hao, Watoa Huduma za Majadiliano ni 222, Wapatanishi 174, Wasuluhishi 37, huku Waendesha Maridhiano wakiwa ni 65.

Katika hatua nyingine, Serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imesajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Hadi Aprili 2025, watoto 10,824,267 wamesajiliwa na kupatiwa vyeti hivyo.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha misingi ya haki za binadamu na utawala bora ambapo Machi 2023, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilipatiwa Daraja “A” na Taasisi ya Kimataifa Inayosimamia Haki za Binadamu Duniani, ikiwa ni kiashiria cha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025, jumla ya Sheria Kuu 57 na Sheria Ndogo 4,087 zimetungwa au kufanyiwa marekebisho, huku Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania ikisajili wanafunzi 5,333, sawa na asilimia 28 ya usajili wa jumla tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008. Katika kipindi hicho, wahitimu 2,375 walimaliza mafunzo na kuingia katika sekta ya sheria kama mawakili.

Vilevile, Chuo cha Uongozi wa Mahakama kimehitimisha jumla ya wanafunzi 2,876 katika kipindi hicho, wakiwemo 1,553 waliohitimu ngazi ya cheti na 1,323 katika ngazi ya astashahada.

No comments:

Post a Comment