SERIKALI YAZIDI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA AFYA YA MSINGI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 24, 2025

SERIKALI YAZIDI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA AFYA YA MSINGI


Na Angela Msimbira


Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeendelea kuboresha huduma za afya ya msingi nchini kwa kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma pamoja na miundombinu muhimu inayosaidia upatikanaji bora wa huduma hizo.

Akizungumza katika kikao kazi cha Maafisa Habari wa Mikoa, Halmashauri na Taasisi kilichofanyika jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa hadi kufikia mwaka 2025, jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka 6,081 mwaka 2020 hadi kufikia 7,735. Ongezeko hilo linajumuisha vituo 1,654 vipya vilivyojengwa katika kipindi cha awamu ya sita ya uongozi wa serikali.

Dkt. Mfaume ameeleza kuwa kati ya vituo vilivyojengwa, zahanati ni 1,158, vituo vya afya ni 367, na hospitali za halmashauri ni 129.

 Aidha, serikali imefanikiwa kujenga zaidi ya nyumba 270 za watumishi wa sekta ya afya ili kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Katika kuimarisha huduma za dharura na uangalizi maalum kwa wagonjwa mahututi, serikali imejenga majengo 87 ya huduma za dharura (EMD) na ICU 30 katika ngazi ya afya ya msingi,” alisema Dkt. Mfaume.

Vilevile, mitambo 21 ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni imewekwa katika hospitali za halmashauri nchini, hatua ambayo imelenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa oksijeni kwa wagonjwa, hasa katika maeneo ya vijijini.

Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wa jamii na kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania wote hadi ngazi ya msingi.

No comments:

Post a Comment