TANZANIA YAVUNA DOLA BILIONI 3.3 KUPITIA SEKTA YA UTALII – WAZIRI DKT. CHANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 13, 2025

TANZANIA YAVUNA DOLA BILIONI 3.3 KUPITIA SEKTA YA UTALII – WAZIRI DKT. CHANA




Na Okuly Julius _ DODOMA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi
Chana , amesema kuwa sekta ya utalii nchini imeingiza mapato ya Dola za Kimarekani bilioni 3.3 kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watalii kufikia 5,360,247, ikiwa ni pamoja na watalii wa ndani 3,218,352 na wa nje 2,141,895.

Dkt. Chana ameyasema hayo leo, Mei 13, 2025, wakati akifungua rasmi Mkutano wa Tatu wa Wizara wa Majadiliano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi katika Utalii (Ministerial Public Private Dialogue - MPPD) uliofanyika Jijini Dodoma.

Akizungumza mbele ya washiriki kutoka sekta mbalimbali, Waziri Chana ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) mwaka 2022.

“Mkutano huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utalii na maagizo ya Mheshimiwa Rais. Wizara yangu imejizatiti kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwenye sekta ya utalii ili kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa,” alisisitiza Waziri Chana.

Ameongeza kuwa juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kukuza utalii, zikiwemo kuimarisha miundombinu, utoaji wa huduma bora na matumizi ya mbinu za kisasa za utangazaji kama vile filamu za Tanzania – The Royal Tour na Amazing Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya World Tourism Barometer ya Januari 2024 kutoka Shirika la Utalii Duniani (UN-Tourism), Tanzania imetajwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kwa ongezeko la watalii wa kimataifa ikilinganishwa na kabla ya janga la UVIKO-19. Pia imeshika nafasi ya 12 duniani kati ya nchi bora zaidi kwa utalii mwaka 2023.

Aidha, Tanzania imepokea tuzo kadhaa za kimataifa zikiwemo Africa’s Leading Destination, World’s Leading Safari Destination, na African Leading Tourism Attraction kwa Mlima Kilimanjaro, huku Bodi ya Utalii Tanzania ikitajwa kuwa bora barani Afrika.

Waziri Chana amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza sekta ya utalii na kutoa wito wa kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha sekta hiyo inatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava amesema mkutano huo ni muhimu kwani inawakutanisha wadau wa sekta ya utalii na uhifadhi na kutoa nafasi ya kutoa mawazo na changamoto inayoikabili sekta hiyo na kuja na Suluhisho la changamoto hizo ili kuendelea kuiboresha.


“Sisi kama bunge tutajitahidi kuendelea kukutana na wadau ili yale mengine ambayo mtakuwa mmeshindwana serikalini au hamjaelewana serikalini au walikosa ujasiri wa kuyasema serikalini basi kwa sisi wawakilishi wao tutakuwa na ujasiri wa kuyasema na kuwasimamia ili mambo yaweze kwenda vizuri", amesema.








No comments:

Post a Comment