Tunakushukuru Rais Dkt. Samia kwa nyongeza ya Mishahara- Naibu Waziri Mwanaidi - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 3, 2025

Tunakushukuru Rais Dkt. Samia kwa nyongeza ya Mishahara- Naibu Waziri Mwanaidi



Na WMJJWM, Dodoma


Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Khamis ametoa shukurani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu kwa nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma ikiwa ni kuongeza chachu katika utekelezaji wa majukumu yao na maendeleo kwa Taifa.

Naibu Waziri Mwanaidi ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo, ambacho kimefanyika Mei 03, 2025 jijini Dodoma.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema maono ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuona watumishi wa umma wanakuwa katika mazingira mazuri ya utendaji kazi wao ili kuleta maendeleo katika Taifa.

Aidha amewasisitiza watumishi kufanya kazi kwa bidii hasa katika kutimiza wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Nitumie fursa hii kuwakumbusha watumishi kuwa hakuna haki bila wajibu, kwa msingi huo nimtake kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma" amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Pia amesizitiza kuwa uongozi wa Wizara utaendelea kutoa motisha kwa watumishi wanaowajibika, wabunifu na wanayoyaishi maadili mema katika Utumishi wa Umma.


Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ameeleza kuwa Baraza hilo ni muhimu kuhakikisha Wizara inatembea pamoja kuhakikisha Dira, Dhima Wizara zinafikiwa na majukumu yanatekelezwa ipasavyo.

"Baraza hili ni chombo muhimu kufikia mafanikio ya Wizara, tulitumie kutathimini jinsi tulivyotekeleza majukumu yetu katika mwaka wa fedha 2024/ 2025 na kujipanga vyema kwa mwaka wa fedha 2025/2026" ameeleza Dkt. Jingu.

Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum limefanyika kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya utendaji kazi na utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 na mipango ya Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2025/2026.






No comments:

Post a Comment