UJENZI NI BAJETI YA KAZI NA UTU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 5, 2025

UJENZI NI BAJETI YA KAZI NA UTU


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewasilisha bungeni bajeti ya wizara yake ambayo imeahidi ujenzi zaidi wa barabara na madaraja nchini – huku akisisitiza uchapakazi zaidi na utu kwenye utekelezaji wa miradi.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma, Ulega amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika eneo la ujenzi kwenye miaka ya karibuni, kazi kubwa itaendelea kufanyika ili kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanafikika katika majira yote ya mwaka.

“Mheshimiwa Spika, tumepiga hatua kubwa katika ujenzi wa barabara na madaraja. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya baadhi ya maeneo kutofikika kwa barabara na mengine yasiyofikika katika majira fulani ya mwaka.

“Katika bajeti hii niliyoiwasilisha leo, ninaomba kuahidi Bunge lako kwamba serikali itaendelea kujenga barabara na madaraja ili kuongeza maendeleo ya taifa letu lakini pia kufanya wananchi wetu waishi maisha ya utu,” alisema Ulega.

Katika maombi yake kwa Bunge, Ulega aliomba wizara ya ujenzi kuidhinishiwa kiasi cha shilingi trilioni 2.28 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Miradi ya Maendeleo.
Baadhi ya vipaumbele vya kimkakati katika bajeti ya mwaka 2025/2026 ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja kwenye maeneo zaidi nchini, kupunguza foleni na misongamano, uwezeshaji makandarasi wazawa, ufungaji taa za barabarani na matumizi ya teknolojia kwenye mizani ili kupunguza usumbufu na rushwa.

Katika hotuba yake hiyo, Ulega alizungumzia suala la utu kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi akisema mara zote alipoagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kuangalia athari kwenye barabara na madaraja, alielekezwa kwanza kuangalia kuhusu hali za watu.

“ Nimeshuhudia kwa macho yangu athari za mvua kuanzia mikoa ya Kusini hadi Morogoro. Jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Rais alikuwa akiuliza kila wakati ni kuhusu usalama wa watu.

“ Tuna mipango yetu na vipaumbele vyetu kama taifa lakini tunaangalia pia utu wa watu wetu. Utu kwa maana kwamba athari kwenye miundombinu zisifanye watu waishi kama si binadamu,” alisema.

Kwenye eneo la mizani, Ulega alisema kuanzia sasa wataanza kufunga kamera maalumu na mashine za kisasa kwenye mizani ambazo hazilazimiki kuendeshwa na watu ili kupunguza makosa ya kibinadamu kwenye utendaji wake.

Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa madereva na watumiaji wa barabara kuhusu rushwa na watu kuzidishiwa uzito na akasema utaratibu mpya utapunguza usumbufu huo.
Katika eneo la uwezeshaji makandarasi wazawa, Ulega alisema serikali imeongeza ukomo wa miradi ya ujenzi wanayotakiwa kupewa makandarasi wa ndani kutoka shilingi bilioni 10 hadi shilingi bilioni 50.

“ Kuanzia sasa, makandarasi wa ndani watapewa kipaumbele kwenye miradi yote ya ujenzi ambayo thamani yake haizidi shilingi bilioni 50. Tuna matumaini kwamba hali hii itaongeza mzunguko wa fedha ndani ya nchi lakini pia uwezo wao wa kujenga miradi mikubwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Ulega alizungumzia pia mpango wa serikali kufunga taa 5,200 pembezoni mwa barabara katika miji zaidi ya 200 nchini ili kupunguza ajali na kuchochea biashara.

Kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025, Mbunge huyo wa Jimbo la Mkuranga, alisema serikali inajivunia kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Magufuli mkoani Mwanza ambalo ujenzi wake sasa umekamilika kwa asilimia 99.

Alisema ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3.2 na litakalokuwa refu kuliko yote kwenye eneo la Afrika Mashariki, utapunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na kusema safari iliyokuwa inatumia zaidi ya saa mbili, sasa itatumia dakika tatu tu.

Pia, alisema kuanza kutumika kwa vivuko vya kampuni ya Bakhresa kwenye eneo la Kigamboni, kumepunguza kwa kiasi kikubwa adha ya usafiri kwa watu waliokuwa wakienda au kutoka Kigamboni.

Mjadala wa bajeti hiyo umeanza jana na utaendelea hadi Mei sita mwaka huu ambapo waziri atafanya majumuisho ya bajeti yake.

No comments:

Post a Comment