Naibu Waziri wa Fedha, Mhe Hamad Hassan Chande (Mb), ameiagiza Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), kuhakikisha sheria na taratibu za michezo hiyo zinafuatwa ili kulinda maadili ya vijana kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ufuatiliaji wa karibu wa michezo hiyo.
Agizo hilo amelitoa bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bagamoyo, Mhe. Muharami Shabani Mkenge, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kusitisha kutoa vibali vya mashine za kamari ili kupunguza umaskini kwa vijana.
Mhe. Chande alisema kuwa hivi karibuni kumekuwepo na wimbi la waendeshaji mashine za sloti pasipo kuzingatia Sheria ya Michezo ya Kubahatisha na sheria nyingine za nchi ambapo waendeshaji haramu huweka mashine zao kwenye makazi ya watu, maduka ya bidhaa, maeneo ya vijijini na pia huruhusu watoto chini ya miaka 18 kushiriki kucheza.
“Ili kukabiliana na michezo ya kubahatisha isiyozingatia Sheria, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha imechukua hatua kadhaa ikiwemo, kusitisha utoaji wa leseni kwa waendeshaji wapya wa mashine za sloti na kuanzisha misako na operation ya kusaka waendeshaji haramu wa mashine za sloti nchi nzima kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kama Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Uhamiaji”, alisema Mhe. Chande.
Alisema kuwa juhudi nyingine zilizofanywa na Bodi hiyo kukabiliana na changamoto hiyo ni pamoja na kuongeza kaguzi za mara kwa mara maeneo mbalimbali ya nchi ilipo biashara ya mashine za slot na kuendesha kampeni inayowalenga vijana na jamii kufanya kazi za uzalishaji na pindi wanapojihusisha na michezo ya kubahatisha basi wacheze kwa kiasi (Responsible gaming).
Mhe. Chande aliliambia Bunge kuwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, imeongeza udhibiti wa uingizaji wa mashine za sloti nchini kwenye maeneo ya mipakani kwa kushirikiana na TRA na imeanza mchakato wa kutumia mifumo ya kielektroniki kudhibiti biashara ya mashine za sloti zinazoendeshwa mitaani (route operation) kama ilivyo kwa michezo mingine ya kubahatisha.
Alisema hatua nyingine ni kuingia makubaliano (MoU) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa lengo la kuwa na ushirikiano wa karibu wa kudhibiti waendeshaji haramu wa mashine za hizo na kupitia mara kwa mara Sheria ya Michezo ya Kubabatisha kwa lengo la kuondoa kasoro na mianya inayotumiwa na waendeshaji haramu wa mashine za sloti.
Aidha, alisema kuwa Bodi inakusudia kutekeleza hatua hizo kikamilifu ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha jamii wakiwemo vijana wanalindwa dhidi ya athari hasi za michezo ya kubahatisha ikiwemo umasikini.
No comments:
Post a Comment