KUELEKEA MACHI 8: WANAWAKE DUWASA WAWASAIDIA WANAFUNZI WENYE UHITAJI BAHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, March 6, 2026

KUELEKEA MACHI 8: WANAWAKE DUWASA WAWASAIDIA WANAFUNZI WENYE UHITAJI BAHI



Na Okuly Julius, OKULY BLOG,BAHI - DODOMA 


Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ifikapo Machi 8, wanawake wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), kwa ufadhili wa Mradi wa VEI DUWASA, wametoa misaada mbalimbali katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, eneo ambalo mamlaka hiyo imekuwa ikitoa huduma za majisafi.

Misaada hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 2.7 imetolewa katika Shule za Msingi Bahi Misheni na Bahi Sokoni, ambapo wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu wamepatiwa vifaa mbalimbali vitakavyowarahisishia katika masomo yao.

Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Meneja wa DUWASA Kanda ya Bahi, Winifrida Masawe, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, amesema msaada huo unalenga kuongeza morali kwa wanafunzi hao ili waendelee kusoma kwa bidii na kufikia malengo yao ya kielimu.

Masawe pia ameushukuru VEI kwa ushirikiano wao katika kufanikisha misaada hiyo inayolenga kurudisha tabasamu kwa wanafunzi hao mbali na misaada mingine ambao wamekuwa wakijitolea katika kusaidia kaya zenye kipato cha chini kupata huduma ya majisafi kwa gharama nafuu ya shilingi elfu thelathini.

Kwa upande wake, Afisa Mahusiano wa DUWASA, Severo Severine, amewakumbusha wanafunzi kutumia maji kwa uangalifu ili kupunguza gharama za bili za maji wanapokuwa majumbani na shuleni na kuwataka kutoa taarifa pindi wanapokuta ubovu wowote katika miundombinu ya maji.

Naye Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Bahi, Idda Shirima, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bahi imeendelea kufanya vizuri kielimu kwa kuongoza mara tano mfululizo katika Mkoa wa Dodoma , huku mwaka jana ikishika nafasi ya kwanza kitaifa katika Halmashauri zilizofanya vizuri katika mitihani ya Darasa la Saba.


Sanjari na hilo, Mwalimu Anna Rose Bwana Mganga ametoa shukrani za dhati kwa DUWASA kwa msaada huo uliolenga wanafunzi wenye uhitaji, uliowahusisha kupatiwa sare za shule, madaftari, kalamu pamoja na taulo za kike.

Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia shule hiyo ya Bahi Sokoni iliyopo Wilaya ya Bahi, Mkoa wa Dodoma, ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
















No comments:

Post a Comment