
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametangaza kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara Mkoani Tanga baada ya Mkandarasi kutoka China kushindwa kutimiza masharti ya mkataba.
Mkandarasi huyo, kampuni ya China Railway 15 Bureua Group anayejenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge) sehemu ya Tungamaa - Mkwaja - Mkange (km 95.2) wilayani Pangani anadaiwa kushindwa kufanya kazi aliyotakiwa kuifanya kwa wakati ingawa tayari amelipwa fedha yote na Serikali.
Baada ya kuvunja mkataba wa awali, Waziri Ulega amemuagiza Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, kuondoa kilometa 25 za barabara hiyo ambazo hajazifanyiwa kazi na badala yake itangazwe zabuni mpya ili wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo wapewe kazi na waanze haraka.
Kufuatia agizo hilo, sasa kilometa 25 za barabara hiyo na kilometa 70 za barabara inayoanzia Mkange hadi Bagamoyo (Makurunge) zitaunganishwa kwenye zabuni ili apatikane Mkandarasi wa kuijenga.
Ulega ametoa maelekezo hayo leo Mei 12, 2025 kwenye ziara yake Mkoani Tanga ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo ambayo Serikali imekwishamlipa Mkandarasi kiasi cha shilingi Bilioni 47 ingawa hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 48 tu.
“Mkandarasi huyu ametuangusha na hapa sisi hadai hata senti kwani tushamlipa zaidi ya bilioni 40, yupo nyuma ya muda, vifaa hajavileta vyote, wafanyakazi hawajawaleta wote, hivyo nimechukua maamuzi ya kumnyang’anya sehemu ya kazi ya mradi ili mradi huu ukamilike kwani ni wa muda mrefu na ni kilio cha wananchi wa Pangani na Mkoa wa Tanga kiujumla”, amesisitiza Ulega.
Ulega ameendelea kusisitiza kuwa maamuzi hayo ya kumyang’anya mkandarasi sehemu ya kazi ni kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi kwasababu Serikali ingeamua kuvunja mkataba wote ingechukua zaidi ya miezi 6 hadi mwaka mzima mpaka Mkandarasi mpya aanze kazi na hasara yake mradi kuendelea kuchelewa.
Vilevile, Ulega amemtaka Mkandarasi huyo kuilipa fidia Serikali kwa kuchelewesha mradi huo ambapo ameielekeza timu wa wataalam kuendelea kuchambua kimkataba juu ya hatua zitakazochukuliwa.
Ulega amemwagiza Katibu Mkuu huyo kumweka mkandarasi huyo katika orodha ya Wakandarasi wasiofanya kazi vizuri katika miradi ya ujenzi kwa siku za usoni ili iweze kusadia wakati wa kupata Makandarasi wengine katika miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.
Kuhusu kilometa 70 ambazo Mkandarasi atatakiwa kuzimalizia, Ulega ameagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuisimamia kampuni hiyo ya China Railway 15 Bureua Group kufanya kazi usiku na mchana ili azikamilishe kuzijenga kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu na ikiwa Wataalamu hao watashindwa kuwasimamia kikamilifu na wao watabadilishwa.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi kutoka TANROADS, Mhandisi Julius Msofe ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 47.82 ikilinganishwa na mpango kazi wa asilimia 100 na kuongeza kuwa muda wa mkataba wa miezi 36 sawa na asilimia 100 umeisha tangu tarehe 31 Machi 2025.



No comments:
Post a Comment