WANAOSIMAMIA MITANDAO YA SERIKALI WATAKIWA KUHAKIKISHA USALAMA WAKE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 21, 2025

WANAOSIMAMIA MITANDAO YA SERIKALI WATAKIWA KUHAKIKISHA USALAMA WAKE



Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa amewataka watumishi wanaosimamia akaunti za mitandao ya kijamii ya Serikali kuongeza umakini na kushirikisha wataalam wa TEHAMA ili kupata elimu ya namna ya kuweka njia za kiusalama katika mitandao hiyo.

Msigwa amesema hayo leo, Mei 21, 2025 wakati akifungua mafunzo ya usalama wa mtandao (cyber security) yalioandaliwa na kitengo cha TEHAMA cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa watumishi wa Wizara hiyo.

Msigwa ameeleza kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya athari za matumizi mabaya ya mtandao zinatokana na uelewa mdogo wa juu ya utumiaji wa mitandao ambapo wengi hawajaweka tahadhari za kiusalama ikiwemo kutobadili taarifa za siri mara kwa mara.

Vilevile Msigwa amesema kuwa, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha usalama wa kimtandao Tanzania ikiwemo uwepo wa sheria ambazo zimetungwa ili kudhibiti matumizi holela ya kimtandao.

Ametaja sheria hizo kuwa ni Sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015 na sheria ya Mamlaka ya Serikali Mtandao ya mwaka 2019 na kuandaa Sera na miongozo mbalimbali ya kusaidia kuhakikisha usalama wa taarifa za Serikali.

Katika hatua nyingine, Msigwa amezitaka taasisi na mashirika ya Serikali kufanya mafunzo hayo ya usalama wa kimtandao mara kwa mara kwa watumishi ili kulinda mifumo na taarifa za Serikali.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA cha Wizara hiyo, Ndg. Kulwa Magingila amewataka watumishi hao kuweka nguvu za pamoja kuhakikisha mitandao ya Serikali inalindwa na kuhakikisha wanatoa taarifa za wanaofanya uhalifu huo kwani ni ajenda ya dunia na uhalifu hauna mipaka.

No comments:

Post a Comment