WAZIRI MBARAWA: SEKTA YA UCHUKUZI YACHANGIA DOLA BILIONI 2.48 KATIKA FEDHA ZA KIGENI NA KUIMARISHA UCHUMI WA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 15, 2025

WAZIRI MBARAWA: SEKTA YA UCHUKUZI YACHANGIA DOLA BILIONI 2.48 KATIKA FEDHA ZA KIGENI NA KUIMARISHA UCHUMI WA TAIFA

Na Okuly Julius- DODOMA 


Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa kwa mujibu wa Taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kati ya Julai 2024 hadi Machi 2025, sekta ya uchukuzi imechangia mauzo ya Dola za Marekani bilioni 2.48, ongezeko la asilimia 8.30 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 2.29 zilizopatikana katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/24.

Amesema mchango huo unadhihirisha nafasi ya sekta ya uchukuzi katika kuimarisha uchumi wa nchi na kukuza sekta ya utalii kupitia huduma za usafirishaji.

Waziri Mbarawa ametoa kauli hiyo leo Mei 15, 2025, Bungeni jijini Dodoma, wakati akitoa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Profesa Mbarawa ameongeza kuwa, mbali na mchango huo wa moja kwa moja katika Pato la Taifa, sekta hiyo pia ni chanzo muhimu cha fedha za kigeni kupitia mauzo ya huduma za uchukuzi (Trade in Services).

"Ongezeko la fedha za kigeni pia linatokana na mapato ya kodi mbalimbali kama vile ushuru wa forodha, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), pamoja na kodi ya mafuta ya petroli na dizeli," ameeleza Profesa Mbarawa.

Amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, Sekta ya Uchukuzi imeendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza na kukuza sekta nyingine za uzalishaji kama vile kilimo, madini, utalii, viwanda na biashara.

"Kwa mujibu wa Taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mwaka 2023, Sekta ya Uchukuzi ilikua kwa asilimia 4.1 na kuchangia asilimia 7.2 katika Pato la Taifa," amesema.

Na kuongeza, "Ukuaji huu umechangiwa pia na kuanza kwa uendeshaji wa reli ya kisasa ya SGR, ambayo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya kitaifa," amesema Mbarawa.

Aidha, ajira zinazotokana na sekta hiyo kupitia shughuli za bandari, usafiri wa majini, barabara, reli na anga zimeendelea kuwa chanzo muhimu cha kipato kwa Watanzania na kuchochea maendeleo ya ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.



BAJETI NA UTEKELEZAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25

Katika mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ya Uchukuzi (Fungu 62) iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,729,676,417,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo. Kati ya kiasi hicho, Shilingi 114,744,476,000 zilitengwa kwa matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi 86,661,930,000 zilitengwa kwa ajili ya mishahara na Shilingi 28,082,546,000 kwa matumizi mengineyo. Hadi kufikia Aprili 2025, jumla ya Shilingi 100,111,641,231.41 sawa na asilimia 87.25 ya bajeti ya matumizi ya kawaida ilikuwa tayari imetolewa.

Kwa upande wa Miradi ya Maendeleo, Shilingi 2,614,931,941,000 zilitengwa, ambapo Shilingi 2,524,369,202,000 ni fedha za ndani na Shilingi 90,562,739,000 ni fedha za nje. Hadi Aprili 2025, jumla ya Shilingi 1,574,336,759,466.90, sawa na asilimia 60.21 ya bajeti ya maendeleo, ilikuwa imetolewa. Fedha hizi zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati kwa lengo la kuimarisha huduma za uchukuzi nchini, kuongeza usalama, kupunguza gharama za usafiri, na kurahisisha biashara ya kikanda na kimataifa.


No comments:

Post a Comment