Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb.), tarehe 24 Mei 2025, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Mchezo wa Gofu unaotekelezwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), eneo la Ihumwa, maarufu kama TPDF Golf Club, jijini Dodoma.
Akizungumza na Maafisa na Askari waliokuwa sehemu ya ziara hiyo, Waziri Dkt. Tax alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo muhimu, ambao watu wengi wamekuwa wakiulizia kuhusu kukamilika kwake na hatua ulipo kufikia kuanza kutumika.
“Ni mradi unaohitaji kusukumwa mbele. Ingawa uhitaji wa fedha ni mkubwa, ni lazima tuhakikishe fedha zinapatikana ili mradi huu muhimu kwa jiji la Dodoma ukamilike. Wageni wengi wanaotembelea Dodoma wamekuwa wakihitaji sehemu nzuri na salama ya kucheza mchezo huu,” alisema Waziri Tax.
Aidha, Waziri Tax aliagiza Kamati ya Ujenzi wa Mradi huo kuhakikisha inakuwa na visima vya maji vya kutosha badala ya kutegemea chanzo kimoja cha maji.
Kuhusu changamoto zinazoathiri utekelezaji wa mradi huo, Waziri Tax aliielekeza Kamati hiyo kuharakisha hatua zinazofuata kwa kuwasilisha nyaraka husika kwenye vikao vya maamuzi ili kupata njia mbadala ya kukamilisha sehemu zilizobakia za ujenzi.
Awali, Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa JWTZ, Meja Jenerali Michael Muhona, alipotoa taarifa fupi kwa Waziri Tax kuhusu mradi huo, alieleza kuwa unajumuisha viwanja 18 vya gofu, hoteli kubwa ya hadhi ya nyota tano, pamoja na viwanja vya michezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mabwawa ya kuogelea na bustani ya wanyama (ZOO). Aliongeza kuwa maandalizi ya viwanja tisa kati ya 18 vimekamilika.
Mara baada ya kukamilika, Uwanja huo wa Kimataifa wa Mchezo wa Gofu wa JWTZ utakuwa ni mkubwa na wa kisasa zaidi kuwahi kujengwa nchini, ukifuatiwa na Uwanja wa TPDF Lugalo Golf Club, ambao pia unamilikiwa na JWTZ. Hii itaifanya JWTZ kuwa taasisi pekee nchini iliyojenga viwanja vyake vya gofu, tofauti na viwanja vingi vilivyopo sasa ambavyo vilijengwa wakati wa enzi za ukoloni.
No comments:
Post a Comment