CRDB Bank Foundation, StartHub Africa zaungana kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 12, 2025

CRDB Bank Foundation, StartHub Africa zaungana kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu


Meneja Uendelezaji Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Sharron Nsule akitoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi walioshiriki semina katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Dar es Salaam, Tanzania – June 2025: Katika kuendeleza jitihada za kuinua ujasiriamali na kuwawezesha wanafunzi wabunifu, Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na StartHub Africa imevitembelea vyuo vikuu vitatu nchini na kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wanaopenda kumiliki biashara baada ya masomo yao.

Ushirikiano huo unaotekelezwa kupitia programu ya “Uni Launch and Scale” tayari umewafikia zaidi ya wanafunzi 1,000 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Iringa na Taasisi ya Uhasibu Arusha (AIA) na kuwapa fursa ya kupata walezi wa kibiashara na mitaji wezeshi kutoka CRDB Bank Foundation.

Akizungumzia mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema vyuo hivi vitatu ni mwanzo tu kwani lengo lililopo ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuwawezesha ili wanapohitimu au wakai wanaendelea na masomo yao waanze kushiriki shughuli za kuujenga uchumi baada ya kuwapa elimu ya fedha, mafunzo ya ujasiriamali na uhakika wa kupata mtaji wezeshi.

“Lengo letu ni kuamsha ari ya ujasiriamali iliyomo ndani ya wanafunzi wetu wa vyuo vikuu na kutoa mazingia rafiki kwao kuanzisha biashara zitakazoajiri vijana wenzao badala ya wao wenyewe kuwa waombaji wa kazi wakihitimu. Kupitia ushirikiano huu tunajenga kizazi cha vijana waliowezeshwa kushiriki kuujenga uchumi wa taifa letu,” anasema Tully.

Katika vyuo vitatu ambako wataalamu wa CRDB Bank Foundation na StartHub Africa wamepita, jumla ya biashara 30 zinazomilikiwa na kuendeshwa na wanafunzi zitachaguliwa baada ya kukaguliwa ili kuingizwa kwenye mpango maalumu wa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji biashara, utayari wa kifedha na utimamu wa bidhaa.

“Kwa kushirikiana na StartHub Africa pamoja na vyuo vikuu hivi, tunaamini tunaendeleza juhudi za kukuza ubunifu hasa wa kidijitali miongoni mwa wanafunzi wetu hivyo kujenga msingi imara wa biashara zinazoweza kukua na kuwanufaisha wananchi wengi,” amesema Tully.

Programu ya Uni Launch and Scale ambayo CRDB Bank Foundation inashirikiana na StartHub Africa kuitekeleza inalenga kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kutekeleza uwekezaji wanaoukusudia kwa kuwapa mafunzo, ulezi wa kibiashara na uwezeshaji wa mitaji kupitia Programu ya Imbeju iliyojielekeza kuwainua vijana, wanawake na makundi maalumu.

Meneja Programu wa StartHub Africa, Zagaro Emanuel anasema katika ushirikiano huu wanakusudia kuwawezesha vijana wengi wabunifu kupitia mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha hivyo kuchangia kuujenga uchumi na kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania.

“Tunawahamasisha wanafunzi na wahitimu wa vyuo vikuu, tunawandaa waanzilishi wapya wa biashara watakaosaidia kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuimarisha ujasiriamali nchini kwa kushirikiana na vyuo vikuu, wawekezaji na wawezeshaji. Tukiwa pamoja na Taasisi ya CRDB Bank Foundation, tunaamini tutafika mbali na kuwajumuisha wanafunzi wengi zaidi nchini,” anasema Emanuel.

Meneja huyo anaongeza kwamba programu hiyo inawapa wanafunzi jukwaa la kujitangaza katika soko la ndani, kitaifa na kimataifa na wanapowasilisha mawazo ya miradi yao, wanajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuvutia mitaji huku vyombo vya habari vikiwarahisishia kujulikana kwa biashara zao hivyo kujiongezea umanifu kwa wadau ambalo ni jambo jema kwa kila biashara.

No comments:

Post a Comment