
Maafisa Habari wa Mikoa wametakiwa kuitangaza kwa nguvu Programu ya Kizazi Chenye Usawa ili kusaidia utekelezaji wa haki na usawa wa kiuchumi nchini.
Wito huo umetolewa leo, Juni 12, 2025, jijini hapa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Wanawake na Makundi Maalum, Bw. Melkion Ndofi, wakati akizungumza katika kikao cha kuwajengea uelewa Maafisa Habari kuhusu utekelezaji wa programu hiyo.
Bw. Ndofi amesema Maafisa Habari ni wadau muhimu katika maeneo yao kwa kuwa ni wasemaji wa miradi mbalimbali ya Serikali. Ameeleza kuwa anaamini kupitia wao, taarifa kuhusu Programu ya Kizazi Chenye Usawa zitasambaa na kufahamika zaidi kwa jamii.
“Programu hii imekuwepo kwa muda mrefu na sasa inatimiza miaka mitano. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alishiriki Mkutano wa Kizazi cha Usawa uliofanyika Paris na akaahidi kuwa kinara katika kutekeleza haki na usawa wa kiuchumi,” amesema Bw. Ndofi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo manne ya kipaumbele ambayo ni, Uwezeshaji wa kijinsia kwenye sekta binafsi, Kazi zenye staha kwa wanawake katika sekta rasmi na isiyo rasmi,Upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji kwa wanawake, na Ubunifu na utekelezaji wa miradi ya kiuchumi kwa wanawake.
“Niwapongeze kwa kujitokeza kushiriki kikao hiki na niwashukuru waajiri wenu kwa kutambua umuhimu wa programu hii. Hii inaonesha wazi kuwa wanathamini nafasi ya habari katika maendeleo,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia katika Wizara hiyo, Bw. Badru Abdnoor, amewataka Maafisa Habari kupaza sauti kuhusu Programu ya Kizazi Chenye Usawa ili jamii ifahamu fursa zilizopo na kuweza kushiriki kikamilifu.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Bi. Juliana Kibonde, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Maafisa Habari, na ndiyo sababu imeamua kuwakutanisha ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu namna bora ya kuitangaza programu hiyo kwa ufanisi.



No comments:
Post a Comment